Wakili Donald Kipkorir kulipwa 1.3Bn katika kesi ya Kaunti ya Nairobi dhidi ya wizara ya ulinzi

Kiasi hicho kimetajwa kuwa kikubwa zaidi katika historia ya uwakili nchini Kenya.

Muhtasari

• Kipkorir alikuwa anawakilisha mteja wake, Kaunti ya Nairobi katika kesi dhidi ya wizara ya ulinzi kuhusu shamba la Embakasi Barracks.

Wakili Donald Kipkorir
Donald Kipkorir Wakili Donald Kipkorir
Image: Facebook

Wakili msomi Donald Kipkorir anatarajiwa kupokea pesa kiasi cha shilingi bilioni 1.3 pesa za Kenya kutokana na kesi aliyoishinda baada ya kuiwakilisha serikali ya kaunti ya Nairobi katika kesi iliyokuwa inaikabili dhidi ya wizara ya ulinzi.

Kesi hiyo ambayo imekuwa kortini kwa muda mrefu ilikuwa imezua vita baridi baina ya uongozi wa kaunti ya Nairobi na wizara hiyo ya usalama, ambapo pande zote mbili zilikuwa zinazozania umiliki wa shamba la ekari 3000 lililotajwa kuwa la thamani ya shilingi bilioni 61.5.

Shamba hilo lililokuwa likizozaniwa na pande hizo lipo katika eneo la Embakasi, sehemu ambayo kambi ya jeshi imejengwa.

Hiki ndicho kiasi kikubwa cha pesa katika historia ya uwakili nchini Kenya kuwahi kupatiwa wakili baada ya kushinda kesi inayomkabili mteja wake.

Kipkorir ameandikisha historia kuwa wakili wa kwanza kabisa nchini Kenya kuwahi kutokea ambaye analipwa kiasi cha juu zaidi katika kesi, na akizungumzia suala hilo la kuandikisha historia ya kipekee, wakili huyo aliwasuta wale wote waliokuwa wakisema kwamba hawezi, na kudhibitisha kweli kwamba chochote chawezekana chini ya jua pakiwepo nia.

“Je, watu wanasema mwana wa Katarina, mke wa nyumbani wa kijijini kutoka Cheptongei na ambaye marehemu baba yake hakujulikana nje ya kijiji hawezi kupata kiasi cha juu zaidi cha pesa katika Historia ya kesi nchini Kenya?” Aliandika Kipkorir kwenye ukurasa wake huku akionekana kuwarushia mafamba wale waliokuwa wakiona kama hangeweza kesi hiyo iliyokuwa inahusisha mamlaka na taasisi za serikali.

Kipkorir ambaye kwa muda mrefu amekuwa akidhihirisha wazi upendo alionao kwa mamake, Katarina, kwa kupakia picha za pamoja mara kwa mara pia alisema kwamba ataendelea na kazi yake ya uwakili na kuwakomesha mahasidi wake huku akishindwa kuwaelewa kama wanataka mawakili wasiweke rekodi za ada katika sheria za kesi.

“Je, wanasema Agizo la Mawakili (Mshahara) linalodhibiti ada lipuuzwe? Je, wanasema tunapuuza sheria ya kesi iliyohusisha ada za kisheria?” aliwauliza wale wote wanaoona kama kiasi alichopewa ni cha juu zaidi kulinganishwa na kazi aliyoifanya.