Uchumi umeporomoka na huku hali ya maisha ikizidi kuwa ngumu, matapeli wanazidi kuongezeka kila sekunde iendayo kwa Mungu, na sasa matapeli si tu watu usiowajua, bali hata mtoto wako vile vile anaweza akakutapei.
Hii ni baada ya taarifa ya kuchekesha na kusitikisha kwa wakati mmoja kupakiwa na maafisa wapelelezi wa jinai DCI kuhusu kisa kimoja ambapo mwanafunzi wa uuguzi alimtapeli mzazi wake kiasi cha elfu 70 pesa za Kenya.
Kulingana na DCI, mwanafunzi huyo anayesomea unesi katika chuo anuwai cha Makindu kwa jina Edwin Kamau mwenye umri wa miaka 23, aliigiza kutekwa nyara kama njia moja ya kutapeli mzazi wake kiasi hicho cha pesa.
“Edwin Kamau ‘alitoweka’ Jumapili iliyopita kabla ya kublock babake na kumpigia simu mamake akidai kutekwa nyara. Alimweleza kuwa watekaji nyara walitaka fidia ya Sh70,000, ili kumwachilia huru kabla ya kukata simu. Wazazi wake waliokuwa wamechanganyikiwa waliripoti kisa hicho kwa maafisa wa polisi ambao mara moja walianzisha msako wa kuwasaka watekaji nyara,” DCI iliripoti.
Hapo ndipo polisi walihaha kweli kweli ili kuokoa maisha ya Kamau huku wazazi wake wakihangaika kuokoa maisha yake kabla ya makataa kuisha. Wazazi walituma kiasi cha elfu 10 na kisha baadae kuongezea kiasi kingine cha elfu 40.
Elfu kumi zilimfikia akiwa na kidosho ambaye walijitoma katika sehemu ya burudani kustarehe kwa pesa hizo.
Polisi wanaripoti kwamba kidosho huyo alikuwa miongoni mwa wale wanaowatilia wanaume vitu vya kuwazuzua kweney vinywaji na baadaye alimwibia Kamau pesa zilizozalia.
Kijana huyo asiye na aibu kwa mara nyingine tena aliwapigia wazazi wake simu kwa kujifanya mtekaji ambapo walituma tena elfu 40 ambazo alificha ndani ya viatu vyake safari hii, lakini wakati huu polisi walikuwa tayari washamvizia kupitia kufuatilia mawasiliano ya simu ile iliyokuwa ikipokezwa pesa.
“Alipohojiwa, Kamau alisema kwamba alikuwa amefuja pesa za karo ya shule ya muhula wake wa mwisho na alikuwa akishangaa jinsi angechangisha pesa za kufanya mitihani yake, hivyo hadithi ghushi ya kutekwa nyara. Aidha alifichua kuwa ‘alitekwa nyara’ pamoja na wanafunzi wengine wawili ambao wazazi wao walikuwa wamelipa fidia,” DCI walieleza.
Kijana huyo alipatikana na kiasi cha elfu 38 alizokuwa amebakisha na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Kayole ambapo anazidi kuhojiwa zaidi kabla ya kufikishwa mahakamani.