Mohammed Ali matatani kwa kuchochea wakulima dhidi ya Brookside ya Kenyatta

Mwezi Machi Mohammed Ali katika kaunti ya Nyeri aliwaambia wakulima Brookside inanunua maziwa kwa shilingi 20 na kuwauzia baadae kwa 120.

Muhtasari

• Kampuni hiyo ilisema matamshi hayo ya Ali yalinuia kuharibu uhusian baina yao na wakulima.

Mbunge wa Nyali Mohammed Ali katika hafla ya kisiasa akisuta Brookside
Mbunge wa Nyali Mohammed Ali katika hafla ya kisiasa akisuta Brookside
Image: Twitter, Maktaba

Kampuni ya kutengeneza bidhaa zitokanazo na maziwa ya Brookside sasa inaarifiwa kumshtaki mbunge wa Nyali Mohammed Ali kwa kile walisema mbunge huyo aliwachochea wakulima dhidi yao.

Katika ripoti zilizosambazwa mitandaoni, Brookside inasemekana kumchukulia hatua za kisheria mbunge huyo mwandani wa naibu rais William Ruto kwa matamshi waliyosema ni uchochezi kwa biashara yao ambapo mnamo mwezi Machi tarehe 3 katika mkutano wa kisiasa kaunti ya Nyeri, Ali anadaiwa kuwaambia wakaazi kwamab Uhuru Kenyatta ambaye ni mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo inayoaminika kumilikiwa na familia kubwa ya Kenyatta anaenda ananunua maziwa kutoka kwa wakulima na baada ya kuiunda anairudisha kuwauzia kwa kiwango cha juu.

Katika makaratasi ya kortini, inasemekana Mohammed Ali alisema Uhuru Kenyatta na familia yake wananunua maziwa kwa shilingi 20 na kisha kuwauzia kwa shilingi 120 baada ya kusindika.

Kampuni hiyo iliyomshtaki Ali ilisema kwamba matamshi hayo ya mbunge wa Nyali yanalenga kuwachochea wakulima kwamba wanadhulumiwa na kuvuruga uhusiano wa kibiashara baina yao na kampuni ya Brookside.

Mohammed Ali kwa muda mrefu amekuwa akitofautiana na rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga huku akimpigia upato naibu rais William Ruto.

Amekuwa akiibua madai kadhaa kuhusu njama ya Raila na Uhuru huku akisema wawili hao wameshikana kuwadhulumu wakenya, na kwa wakati mmoja aliwahi sema wamevuruga shughuli zilizokuwa zikiendeshwa katika bandari ya Mombasa huku akimrushia kidole cha lawama gavana wa Mombasa Hassan Joho kwa kile alisema ni kuwasaliti wana pwani kwa kukaa kimya wakati bandari inavuliwa mamlaka ya kuendesha shughuli nyingi kama hapo awali kabla ya ujio wa reli ya kisasa ya SGR.