Mwanaume ashtakiwa kwa kupiga na kujeruhi wanawe mapacha wa miezi 6

Mama yao alienda kwa jirani na kurudi akapata watoto wanalia kwa uchungu ambapo Okello pia alimpiga na kumzuia kuwapeleka hospitali.

Muhtasari

• Mapacha hao wamelazwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta.

Fredrick Okello katika mahakama ya Kibera ambapo alishtakiwa kwa madhara makubwa
Fredrick Okello katika mahakama ya Kibera ambapo alishtakiwa kwa madhara makubwa
Image: CLAUSE MASIKA (The Star)

Mwanaume mmoja alifikishwa katika mahakama ya Kibera kwa kosa la kuwapiga na kuwajeruhi vibaya watoto wake mapacha wa miezi 6.

Mwanaume huyo aliyetambulika kwa jina Fredrick Okello, 24, ilisemekana aliachiwa watoto na mama yao ambaye aliondoka kwenda kwa Jirani na aliporudi akapata pacha wa kiue analia kwa maumivu makubwa.

Mama watoto alipojaribu kuuliza tatizo, pia Okello alimpokeza kichapo na hata kumzuia ndani ili asiwapeleke watoto hospitalini.

Kitendo hicho kilitokea mnamo tarehe 6 Julai katika makaazi yao eneo la mtaa wa mabanda wa Raila na mahakama ilijulishwa kwamba mapacha hao bado wamelazwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Mwendesha mashtaka Nancy Kerubo aliiambia mahakama kwamba mmoja wa mapacha hao alivunjika mguu na hivyo kuitaka mahakama kumzuilia mshtakiwa kwa siku nyingine zaidi bil kumpa dhamana.

Mshtakiwa alikana mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi Esther Bhoke katika Mahakama ya Kibera. Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 bila chaguo la dhamana ya pesa taslimu. Kesi hiyo itatajwa Julai 26, 2022.