Wazazi washtakiwa kwa madai ya kumwaga Maji moto kwenye makalio ya Mtoto

Muhtasari

• Washtakiwa walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Kibera Monica Maroro ambapo walikanusha mashtaka.

• Maafisa walikimbilia eneo la tukio na walipofika walimkuta mvulana huyo akihema kwa maumivu.

Irene Nduku katika mahakama ya Kibera ambapo alishtakiwa kwa kosa hilo pamoja na mumewe. Picha: CLAUSE MASIKA
Irene Nduku katika mahakama ya Kibera ambapo alishtakiwa kwa kosa hilo pamoja na mumewe. Picha: CLAUSE MASIKA
Image: PICHA CLAUSE MASIKA

Mwanamume na mkewe wanashtakiwa kwa kusababisha majeraha mabaya kwenye makalio ya mvulana wa miaka minne walishtakiwa katika mahakama ya Kibera.

Mnamo Alhamisi, Samuel Adega na Irene Nduku walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Kibera Monica Maroro ambapo walikanusha madai hayo.

Hati ya mashtaka ilisema kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa tarehe tofauti kwa wakati usiojulikana katika eneo la Parklands, Kaunti Ndogo ya Westlands ndani ya kaunti ya Nairobi.

Nduku ambaye ni mama mzazi wa mtoto huyo alisomewa shtaka tofauti la pili la kukiuka haki ya mtoto kwa kukataa kumpatia dawa mtoto huyo.

Alikanusha shtaka la tatu la kushindwa kumlinda mtoto dhidi ya unyanyasaji wa kimwili kulingana na sheria.

Kulingana na ripoti ya polisi, walipokea simu kuwajulisha kuwa kuna mtoto ambaye alionekana kana kwamba alikuwa amenajisiwa.

Maafisa hao walikimbilia eneo la tukio na walipofika walimkuta mvulana huyo akihema kwa maumivu.

Ripoti ya polisi inasema kuwa mtoto huyo alisema alichomwa na maji ya moto makalio.

Alikimbizwa hospitalini ambako alitibiwa na kupelekwa kwenye nyumba ya watoto.

Baadaye wazazi hao walikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi kabla ya kufikishwa mahakamani.

Washtakiwa hao waliiomba mahakama kuwaachilia kwa  bondi nafuu kupitia kwa wakili wao.

Wakili huyo aliambia mahakama kuwa mshtakiwa hakuwa na uwezo wa kulipa masharti magumu ya bondi.

Sambamba na hilo, mahakama ilikataa kumruhusu mama huyo kumtembelea mvulana huyo kama alivyoomba.

Akizungumza kupitia kwa wakili huyo, mama huyo aliiambia mahakama kuwa mvulana huyo alikuwa kwenye nyumba ya watoto na kwamba anakosa upendo wa mama.

Akijibu, Maroro alikataa ombi hilo na kuwataka wawe mbali na mtoto huyo hadi wapate mwelekeo kutoka Kortini.

Pia aliwaachilia kwa bondi ya Sh500,000 na kuagiza kwamba suala hilo litasikizwa  baadaye  mwishoni mwa mwezi huu.