Mwalimu ashtakiwa kwa kunajisi mwanafunzi aliyeenda kuchukua karatasi za mtihani kwake

Mshtakiwa alifanya kitendo hicho baada ya msichana huyo kwenda nyumbani kwake kuchukua karatasi za zamani.

Muhtasari

•Sammy Kipkemoi Melly alishtakiwa katika mahakama ya Kibera kwa kumnajisi msichana wa shule mwenye umri wa miaka 14.

•Mshtakiwa anadaiwa  kufanya kitendo hicho baada ya msichana huyo kwenda nyumbani kwake kuchukua karatasi za zamani.

Sammy Kipkemoi Melly katika mahakama ya Kibera
Sammy Kipkemoi Melly katika mahakama ya Kibera
Image: CLAUSE MASIKA

Mwalimu mmoja ameshtakiwa katika mahakama ya Kibera kwa kumnajisi msichana wa shule mwenye umri wa miaka 14, kinyume na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana.

Sammy Kipkemoi Melly alishtakiwa mbele ya hakimu mkuu mwandamizi wa Kibera Phillip Mutua ambapo alikanusha mashtaka.

Karatasi ya mashtaka inasema kuwa kosa hilo lilitekelezwa kwa tarehe tofauti kati ya Oktoba 2021 na Julai 2022 katika hifadhi za maji za Nairobi, kaunti ndogo ya Lang’ata ndani ya Kaunti ya Nairobi.

Pia alishtakiwa kwa kosa la pili la kufanya kitendo kisicho na heshima na mtoto mdogo, kinyume na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana.

Maafisa wa upelelezi wanasema kuwa mshtakiwa alifanya kitendo hicho baada ya msichana huyo kwenda nyumbani kwake kuchukua karatasi za zamani.

Mshukiwa alikanusha mashtaka na, kupitia wakili wake, akaiomba mahakama kumwachilia kwa dhamana ya pesa taslimu.

Wakili huyo aliitaka mahakama kumpa mteja wake muda wa dhamana, akisema kuwa mshtakiwa si hatari ya kukimbia.

Hakimu alimwachilia mshukiwa kwa bondi ya Sh300,000 na kuagiza kwamba kesi hiyo itajwe baadaye mwezi huu.