Mahakama yazungumzia madai kuwa iliamuru mwanadada kulipa 23,750 kwa kula fare ya 3000

Jamaa anadaiwa kumtumia mpenziwe nauli ya Ksh3000 ili afanya mpango wa kuhudhuria ila akakosa kufika.

Muhtasari

•Jamaa mmoja ambaye alikuwa ameandaa karamu ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa alimtumia mpenzi wake nauli ya Ksh3000 ili afanya mpango wa kuhudhuria ila akakosa kufika.

•Ilidaiwa mwanadada huyo aliagizwa kurejesha Sh3000 alizopokea pamoja na riba ya Ksh750 na faini ya Ksh kwa ajili ya madhara ambayo alimsababishia.

Mahakama
Mahakama

Idara ya Mahakama nchini Kenya imepuuzilia ripoti kwamba mwadada mmoja aliagizwa kumlipa mpenziwe Ksh 23, 750 kwa madai ya kutumia pesa alizotumiwa kama nauli.

Ripoti iliyoenezwa kwenye mitandao ya kijamii ilidai kwamba jamaa mmoja ambaye alikuwa ameandaa karamu ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa alimtumia mpenzi wake nauli ya Ksh3000 ili afanya mpango wa kuhudhuria ila akakosa kufika. 

"Mwanaume huyo alienda katika mahakama ya madai madogo na kuwasilisha kesi pamoja na ushahidi unaojumuisha taarifa yake ya M-pesa na mazungumzo ya WhatsApp kati yake na mpenziwe ya kabla na baada ya kutuma pesa hizo baada ya bibi huyo kupuuza jumbe zake na kisha kuzima simu yake," Ripoti hiyo ilisoma.

Ilidaiwa kuwa mahakama ya madai madogo ya Milimani iliamuru mwanadada huyo arejeshe Sh3000 alizopokea kutoka kwa mpenzi wake pamoja na riba ya Ksh750 na faini ya Ksh kwa ajili ya madhara ambayo alimsababishia.

"Mwanamke huyo alizuiliwa akisubiri malipo ya uharibifu na familia yake," Ripoti ilisoma.

Idara ya mahakama hata hivyo imejitokeza na kupuuzilia mbali ripoti hiyo huku ikiweka wazi kuwa ni ghushi.

"Habari za uwongo!" Idara ya mahakama imesema kupitia mtandao wa Twitter.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko ni mmoja wa walianguka kwenye mtego wa ripoti hiyo ya uwongo na kuisambaza.

Sonko alisambaza ripoti hiyo kupitia Facebook na kudokeza kuwa amewahi kutuma nauli kwa wanadada zaidi ya 5000 na wakaila.

"Kumbe siku hizi dame akila fare yako unaweza kumpeleka mahakamani ili pesa zako zirudishwe pamoja na riba. Nimeona habari hii ambayo ilifanyika jana... Hii ingekuwa zamani ningeweka ndani zaidi ya wanadada 5000," Sonko aliandika Alhamisi.

Wanamitandao wengine pia waliamini taarifa hiyo na kuisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.