Mtoto wa miaka 15 akamatwa kwa kuwaua ndugu zake watatu na binamu mmoja

Mtoto huyo sasa anashikiliwa katika kituo hicho akisubiri kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

Muhtasari

• Msichana huyo muuaji aligundulika na maafisa wa polisi baada ya babake kupiga ripoti katika kituo cha polisi cha Kikuyu

DCI wamemtia mbaroni mtoto wa miaka 15 kwa kuua watu 4
DCI wamemtia mbaroni mtoto wa miaka 15 kwa kuua watu 4
Image: MAKTABA

Kitengo cha maafisa wa upelelezi wa jinai, DCI kimeelezea taarifa moja ya kusikitisha jinsi mtoto wa miaka 15 alishiriki mauaji ya ndugu zake wadogo watatu katika kaunti ya Kiambu.

Mtoto huyo ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza alielezea taarifa ya kugandisha damu jinsi aliwaua ndugu zake watatu pamoja na binamu yake katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Mtoto huyo alikuwa akitoa ufichuzi huu wa hadithi ya kusadikika jinsi aliua watatu hao wa miezi 15, miaka 5 na miaka 7 chini ya mwaka mmoja uliopita pamoja na binamu yake aliyekuwa na miezi 20 katika Kijiji cha Gatiga eneo la Kabete, mauaji ambayo aliyatekeleza mwezi mmoja uliopita baada ya kumtumbukiza mtoto huyo kwenye kisima kilichokuwa na maji.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa na DCI kwenye ukurasa wao wa Facebook, msichana huyo muuaji aligundulika na maafisa wa polisi baada ya babake kupiga ripoti katika kituo cha polisi cha Kikuyu ambaye alimtuhumu kwa kuwaua wadogo zake, jambo ambalo baadae lilitokea kuwa la kweli baada ya msichana huyo kufunguka ukweli wake kituoni humo.

“Mapema leo, babake msichana huyo aliyejawa na huzuni alitembea hadi kituo cha polisi cha Kikuyu na kurekodi ripoti dhidi ya msichana huyo wa miaka 15 ambaye alimtuhumu kuwaua wadogo zake watatu. Mtoto huyo alikiri kutekeleza mauaji hayo mbele ya afisa wa watoto katika kaunti ndogo ya Kikuyu,” DCI iliripoti.

Mtoto huyo sasa anashikiliwa katika kituo hicho akisubiri kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

Kisa hiki kinawiana na kile cha kijana Lawrence Warunge, kijana wa chuo kikuu katika kaunti hiyo hiyo ya Kiambu ambaye alikiri kutekeleza mauaji ya wanafamilia wake wanne, wakiwemo wazazi wake na ndugu zake wawili pamoja na mfanyikazi wa shambani, katika kile alitaja kwamba alipata motisha kutoka kwa filamu moja ya mauaji mnamo mwaka 2021 Januari katika eneo la Kiambaa.

Baadae kijana huyo alipatikana kuwa na akili isiyo timamu na kesi hiyo ikasitishwa kwa muda ili kumpa nafasi ya kupata nafuu kabla ya kushtakiwa mahakamani.