logo

NOW ON AIR

Listen in Live

DPP abadili ombi la kutaka kusitishwa kwa kesi dhidi ya aliyekuwa Gnamam Lenolkulal

Stakabadhi za mashtaka zaonyesha kuwa Lenolkulal ‘alijinufaisha kibinafsi moja kwa moja

image
na Davis Ojiambo

Habari14 October 2022 - 09:28

Muhtasari


  • • Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma siku ya Jumatano ilitaka kuondoa kesi ya ufisadi wa Shilingi milioni 84 inayomkabili gavana huyo wa zamani.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji

DPP ameondoa ombi lake lililokuwa likitaka kutupilia mbali mashtaka dhidi ya aliyekuwa Gavana wa Samburu Moses Lenolkulal. 

Msaidizi Mwandamizi wa DPP Alexander Muteti siku ya Ijumaa aliambia mahakama kwamba walikuwa wamewasilisha ombi la kutaka kesi hiyo iondolewe lakini baada ya kushauriana zaidi na DPP Noordin Haji, wameamua kuondoa ombi hilo. 

Muteti alisema kesi hiyo inapaswa kuendelea kama ilivyopangwa hapo awali. Hakimu Thomas Nzioki aliruhusu ombi la DPP. Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Januari 23, 2023, wakati shahidi wa mwisho anatarajiwa kufika kizimbani. 

Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma siku ya Jumatano ilitaka kuondoa kesi ya ufisadi wa Shilingi milioni 84 inayomkabili gavana huyo wa zamani wakati kesi hiyo inaelekea kukamilika. 

Hii ilikuwa baada ya Lenolkulal kuwasilisha ombi kwa afisi yao akitaka kuchunguzwa upya kwa mashtaka hayo, akisema alikuwa akichukua hatua zinazofaa kuachilia umiliki wake katika kampuni ya mafuta ya Oryx Service Station. 

Lenolkulal alishtakiwa mwaka wa 2019 katika mahakama ya Milimani kwa makosa manne ya matumizi mabaya ya na kusababisha kupotea kwa pesa za umma milioni 84. Ameshtakiwa kwa kutumia kampuni yake-Oryx service station-kusambaza mafuta ya petroli na dizeli katika kaunti hiyo. 

Stakabadhi za mashtaka zaonyesha kuwa Lenolkulal ‘alijinufaisha kibinafsi moja kwa moja katika mikataba kati ya Oryx na kaunti ya Samburu kwa usambazaji wa mafuta”. Mashtaka hayo yanamkabili yeye Lenolkulal, Hesbon Ndathi na watu wengine tisa. 

Lenolkulal katika ombi lake DPP alidai kuwa mawasiliano kutoka kwa serikali ya kaunti ya idara ya hazina ya Samburu ilionyesha hakuna ukiukaji wa ununuzi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved