logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mombasa: Mraibu wa bangi ashtakiwa kwa kuwacharaza polisi kwa fimbo

Nasoro aliwashambulia polisi ambapo alimjeruhi mmoja miguu yote na mwingine mkono.

image
na Davis Ojiambo

Habari02 November 2022 - 07:45

Muhtasari


  • • Mahakama ilielezwa kwamba maafisa hao walikuwa wakishika doria kwa miguu mwendo wa saa 3:20 usiku.

Jumanne mwanaume mmoja jijini Mombasa alishtakiwa kwa kosa la kuwashambulia polisi wawili.

Kulingana na jarida la Nation, polisi hao wawili walikuwa wanafanya doria katika sehemu ya Kibokoni wakati walikutana na mwanaume huyo na kutaka kumsaili wakati walipatana na harufu kali ya dawa ya kulevya aina ya bangi.

Badala ya kumfanyia usaili, mwanaume huyo kwa jina Salim Nasoro aliwageuzia polisi kibao na kuwashambulia kwa fimbo ambapo alimpiga mmoja miguuni na mwingine kwenye mmoja wa mkono wake.

“Mahakama ilielezwa kwamba maafisa hao walikuwa wakishika doria kwa miguu mwendo wa saa 3:20 usiku katika eneo la Old Port walipokutana na mshukiwa akiwa na fimbo. Askari hao waliokuwa wamevalia kiraia, inadaiwa walimsimamisha Bw Nasoro na kujitambulisha na kuanza kumhoji. Walishuku kwamba alikuwa ametoka tu kuvuta bangi,” Nation waliripoti.

Walimuuliza kwa nini alikuwa akizurura na fimbo. Mshukiwa huyo anadaiwa kuwa mkali na kuanza kuwachapa viboko maafisa hao mmoja baada ya mwingine.

Lakini maafisa hao walimzidi nguvu mshukiwa, wakampiga mweleka chini na kumfunga pingu kabla ya kumsindikiza hadi Kituo Kikuu cha Polisi.

Maafisa hao kisha walikwenda kwenye zahanati iliyokuwa karibu kwa matibabu na walipewa fomu za P3 (kwa ajili ya kuripoti shambulio hilo).

Bw Nasoro alifika mbele ya Hakimu Mkuu wa Mombasa Martha Mutuku na kukana kutenda makosa hayo.

Aliachiliwa kwa bondi ya Sh 200,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho au dhamana mbadala ya pesa taslimu Sh100,000. Kesi hiyo itatajwa Novemba 17.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved