Mwanamume azuiliwa rumande siku 14 kwa madai ya kumuua mpenziwe

Askari polisi walitembelea eneo la tukio na kukuta mwili wa marehemu ukiwa umefunikwa kwa shuka kwenye sofa

Muhtasari
  • Damu nazo zilionekana ukutani na sakafuni jambo ambalo lilikuwa ni dalili ya mapambano katika eneo la tukio
THOMAS MBUGUA MUTHEE AKIWA KWENYE MAHAKAMA YA KIBERA
Image: CLAUSE MASIKA

Mwanamume anayeshukiwa kumuua mpenzi wake huko Lang'ata baada ya kutofautiana kwa muda mfupi amezuiliwa kwa siku 14 akisubiri uchunguzi ukamilike.

Thomas Mbugua Muthee alizuiliwa na hakimu mkuu mwandamizi wa Kibera Monica Maroro baada ya wakili wake kuambia mahakama kuwa hawapingi hati ya kiapo ambayo afisa wa upelelezi aliwasilisha kortini aliyetaka maagizo ya kumzuilia.

"Hatuna tatizo na maombi ya kumweka kizuizini mlalamikiwa, lakini tunaomba tarehe ya mapema iwezekanavyo," alisema wakili wake.

Wakati akiwasilisha ombi hilo mahakamani, Inspekta Nicolas Langat aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa alikuwa hatarina anaweza kutoweka.

“Tulimkamata baada ya juhudi za pamoja na baadhi ya maafisa wa DCI kutoka Uganda. Alikamatwa katika mpaka wa Malaba alipokuwa akijaribu kutoroka,” aliambia mahakama.

Alisema kuwa mshtakiwa anashukiwa kumuua Naneu Muthoni usiku wa Novemba 2022 katika eneo la Onyonka katika kaunti ndogo ya Lang'ata.

"Kwamba mlalamikiwa alionekana mara ya mwisho akiwa na marehemu kwenye nyumba yao ya kupanga usiku wa Novemba 12 ambapo inadaiwa kulikuwa na majibizano kati ya wawili hao na ghafla kila kitu kilinyamaza," mahakama ilisikiza.

Askari polisi walitembelea eneo la tukio na kukuta mwili wa marehemu ukiwa umefunikwa kwa shuka kwenye sofa huku ukiwa na majeraha ya kukatwa kichwani.

Damu nazo zilionekana ukutani na sakafuni jambo ambalo lilikuwa ni dalili ya mapambano katika eneo la tukio.

Mahakama iliamuru mshukiwa arejeshwe rumande na upelelezi ukamilike kwa wakati.