Kamagera aliyetumia fujo kuitisha Ksh 20 kutoka kwa manamba wa matatu kuhukumiwa

Mwanaume huyo wa kujaza abiria kwenye gari alizua rabsha katika mtaa wa Kayole alipotaka kupewa Ksh 20 kabla ya kuruhusu gari kubeba abiria katika steji hiyo.

Muhtasari

• Kamagera ni wale watuvambao aghalabu hupatikana katika steji za matatu ambao husaidia makanga wa matatu kujaza abiria kabla ya kuitisha pesa kwa kazi hiyo.

Mwanaume aliyekamatwa
Mwanaume aliyekamatwa

Mwanaume mmoja aliyeitisha chenji ya shilingi ishirini kutoka kwa manamba wa matatu moja jijini Nairobi anasubiria kuhukumiwa baada ya kukiri makosa yake.

Mwanaume huyo alikuwa anadanganya kuwa manamba wa matatu hiyo hakuwa amemrudishia chenji yake kumbe alikuwa anataka kumlaghai na pia kumtukana matusi ya kila rangi, jambo lililovutia fujo kali baina yao.

Kulingana na taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Bw Stanley Thuita alikiri katika Mahakama ya Makadara kwamba alidai pesa hizo kutoka kwa Samuel Kanja wa Forward Travelers Sacco katika steji ya Mihango eneo la Kayole, Nairobi akitishia kumpiga mnamo Novemba 8.

Bw Thuita pia anakabiliwa na mashtaka ya kujiendesha kwa njia ambayo huenda ikasababisha uvunjifu wa amani. Anadaiwa kutumia lugha ya matusi kwa msimamizi wa sacco hiyo Bw Peter Mwangi ambaye aliingilia kati mshtakiwa na kundi la watu wakimzunguka Bw Kanja.

Bw Thuita na wengine ambao hawakufika kortini wanaripotiwa kukabiliana na Bw Kanja wakitaka pesa kutoka kwake, ambapo walitishia kutomruhusu kuchukua abiria kutoka jukwaani.

 

Wakati wa kisa hicho, mshtakiwa na wenzake ambao wanafanya kama ‘kamagera’ kwa lugha ya mtaani walifunga mlango wa matatu kwa nguvu na kuwazuia abiria kupanda.

Kamagera ni wale watuvambao aghalabu hupatikana katika steji za matatu ambao husaidia makanga wa matatu kujaza abiria kabla ya kuitisha pesa kwa kazi hiyo.

Bw Kanja na dereva wake walimpigia simu afisa wa sacco ambaye alimwarifu Bw Mwangi na wawili hao wakapanda jukwaani ili kujua kilichokuwa kikitendeka.

Bw Thuita alikiri mashtaka yote mbele ya Hakimu Mkazi Mercy Thibaru. Kesi hiyo itatajwa kwa ajili ya kusomewa ukweli kwa mtuhumiwa kabla ya kutiwa hatiani na kuhukumiwa.