Aliyefungwa maisha gerezani ahukumiwa miaka mingine 35 kwa kumuua mfungwa mwenzake

Peter Hiuhu Gachau almaarufu Undertaker alimpiga mfungwa mwenzake kwa nyundo aliyoiingiza gerzani kutoka kwa duka la mafunzo ya useremala.

Muhtasari

• Kifungo chake cha miaka 35 juu ya kifungo cha maisha kiliafikiwa na jaji kutokana na ushahidi kwamba marehemu aliuawa akiwa amelala.

Mfungwa akiwa jela
Mfungwa akiwa jela
Image: Mfungwa Jela

Peter Hiuhu Gachau, mwanaume aliyehukumiwa kifungo cha maisha katika gereza la King’ong’o kaunti ya Nyeri kwa mara nyingine amepatikana na hatia ya kumuua mfungwa mwenzake miaka 7 iliyopita na kuhukumiwa miaka 35 jela.

Kulingana na Jarida la Nation, Gachau alifikishwa mbele ya jaji wa mahakama kuu Florence Muchemi, alipatikana na hatia ya kumuua mfungwa mwenzake kwa jina Shem Mugendi usiku wa Agosti 17 miaka 7 iliyopita.

Gachau anafahamika gerezani na wenzake kwa jina la Undertaker.

Kifungo chake cha miaka 35 juu ya kifungo cha maisha kiliafikiwa na jaji kutokana na ushahidi kwamba marehemu aliuawa akiwa amelala.

“Kitendo cha mshtakiwa lazima kilisababisha hasara na uchungu mkubwa kwa mwathiriwa, ambaye pia alinyongwa na kufungwa pingu alipokuwa amelala. Mahakama ilikuwa imegundua kuwa Gachau alimpiga Mugendi mara kadhaa kwa nyundo ambayo alikuwa ameingia kisiri kutoka katika karakana alimokuwa akisomea useremala,” Nation walimnukuu jaji Muchemi.

Waendesha mashtaka walikuwa wamependekeza kifungo cha maisha kwa Gachau, wakisema kwamba hakuwa amebadilisha tabia yake ya jeuri.

Walisema Gachau alikuwa akitumikia kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa mabavu na mahakama ya Nyeri mnamo mwaka 1999.

Mahakama ilikuwa imemhukumu kifo lakini kifungo chake kikabadilishwa na kuwa maisha kufuatia agizo la rais kipindi hicho, hayati Mwai Kibaki.