Jamaa akiri kosa la kukata miti katika Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi

Gicheru alitozwa faini ya Sh10,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita jela.

Muhtasari

•Samuel Gicheru alikiri mashtaka mbele ya hakimu mkuu mwandamizi wa Kibera Esther Boke siku ya Jumatano.

•Aliiambia mahakama kuwa alijuta sana, lakini akadai yeye ni maskini na ni mtu mwenye familia.

Samuel Gicheru katika mahakama ya Kibera
Image: CLAUSE MASIKA

Mwanamume mmoja amekiri kosa la kuiba miti katika Hifadhi ya Kitaifa ya Nairobi.

Samuel Gicheru alikiri mashtaka mbele ya hakimu mkuu mwandamizi wa Kibera Esther Boke siku ya Jumatano.

Gicheru alishtakiwa kwa kukata miti ya Acacia mnamo Januari 14 kando ya barabara ya Southern Bypass.

Kulingana na upande wa mashtaka, Gicheru alikamatwa na maafisa ambao walikuwa wakishika doria.

 "Maafisa hao walimwona akikata miti na akaamriwa kukomesha alichokuwa akifanya kwani ilikuwa kinyume cha sheria katika eneo lililohifadhiwa," mahakama ilisikiza.

Aliiambia mahakama kuwa alijuta sana, lakini akadai yeye ni maskini na ni mtu mwenye familia.

Gicheru alitozwa faini ya Sh10,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita jela.