"Mimi ni mdogo sana kuenda jela!" Jambazi aliyependa aliyemuibia aiambia Korti

Matundura mwenye miaka 24 alimpenda msichana mmoja katika nyumba ambayo walienda kuiba mnamo mwaka 2017.

Muhtasari

• Kipindi hicho akiwa na miaka 19, alivutiwa na msichana mmoja katika nyumba walimoiba na kuomba kubadilishana namba.

Mfungwa akiwa jela
Mfungwa akiwa jela
Image: Mfungwa Jela

Kijana mmoja aliyepatikana na hatia ya wizi wa kimabavu baada ya kumpenda mmoja wa wenye nyumba ambayo yeye na genge lake walifanya uvamizi, ameiomba mahakama kumpa msahama wa kutomfunga jela katika kile alisema kuwa yeye bado ni mdogo sana kufungwa.

Kevin Matundura mwenye umri wa miaka 24 pamoja na genge lake walivamia boma moja katika kaunti ya Nakuru mwaka 2017 lakini walipokuwa wanamaliza shughuli yao ya kuwaibia wenye nyumba, alivutiwa na kidosho mmoja kweney nyumba hiyo na kuomba wakabadilishane nambari za simu.

Baadae alianza kumtongoza kwa meseji za simu, jambo ambalo lilipelekea kukamatwa kwake pamoja na wenzake, baada ya polisi kutumia msichana huyo ili kumfikia mtuhumiwa.

Kesi yao imekuwa ikiendeshwa na mapema wiki jana, walipatikana na hatia ya wizi wa kimabavu ambapo walitarajiwa kuhukumiwa kifungo.

Lakini akijitetea mbele ya hakimu mkuu mkaazi wa mahakama ya Nakuru Jumatatu ya Januari 23 ambapo hukumu yao ilikuwa itolewe, Matundura alimuomba hakimu kumpa msamaha wa kutofungwa jela, akisema kuwa umri wake bado ni mdogo sana kuanza kuhudumia kifungo jela, huku akijutia kitendo chake.

“Niko katika umri mdogo na sitaki kukaa kizuizini maisha yangu yote. Nimepitia ushauri nasaha na ningependa niruhusiwe kurudi nyumbani na kurudisha kwa jamii,” alisema Matundura.

Katika kisa cha wizi kilichotokea usiku wa Machi 14, 2017, Matundura mwenye umri wa miaka 19 kipindi hicho na Wainaina walikuwa miongoni mwa genge la wanaume wanne waliovamia nyumba ya Bw James Wamugunda, mfanyabiashara na mkulima katika kaunti ndogo ya Bahati.

Hukumu hiyo iliyokuwa imepangwa Jumatatu ilikosa kufanyika baada ya mahakama kufahamishwa kuwa ripoti ya awali ya dhamana haikuwa tayari.

Mahakama iliahirisha hukumu hiyo hadi Februari 6.