Eldoret: Kesi ya mvulana (14) aliyemuuwa mpwa wake (6) kusuluhishwa nje ya mahakama

Inaarifiwa mvulana huyo alimuuwa mpwa wake kwa kumpiga fimbo kichwani baada ya kudai kwamba aligoma kufanya "homework"

Muhtasari

• Mshtakiwa alimuua mpwa wake usiku wa Agosti 28, 2022 katika kijiji cha Moiben katika kaunti ndogo ya Moiben.

Mahakama
Mahakama
Image: MAHAKAMA

Familia ya mvulana wa miaka 14 aliyemuua mtoto wa kakake mkubwa kwa sababu ya kazi ya ziada ya shuleni ameiomba mahakama ya Eldoret kuruhusu wahusika kupata suluhu ya kesi hiyo nje ya mahakama.

Kulingana na wajuzi wa sheria, kesi zinazohusisha watoto wa chini ya miaka 18 aghalabu huombwa kutafuta suluhu nje ya mahakama kwa dhana kwamba bado ni watoto na huenda hawajapata uelewa wa sheria wanapotekeleza makosa.

Mtoto huyo alikamatwa na maafisa wa polisi kutoka Moiben. Alipohojiwa, alikiri kwamba alimuua kwa bahati mbaya mpwa wake wa miaka sita baada ya kupigana kwa ajili ya kazi za ziada za shuleni, wakiwa nyumbani, jarida moja liliripoti.

Mshitakiwa huyo alisema mtoto mdogo wa kaka yake aligoma kufanya kazi zake za nyumbani na kumpiga na fimbo kichwani na kusababisha kuzimia. Mtoto huyo alifariki kutokana na jeraha la kichwa alipofika katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH) ambapo alikimbizwa kwa matibabu.

Kupitia wakili wake Loureen Isiaho, mwanafunzi wa darasa la saba aliiambia mahakama kwamba wanafamilia walijadili suala hilo na wako tayari kukumbatia usuluhishaji nje ya korti.

Wakili wa Serikali hakupinga maombi ya washtakiwa hao, badala yake aliiomba mahakama kuwaruhusu pande zote kukutana na upande wa mashtaka pamoja na wakili wao kwa ajili ya kuendelea na maombi hayo.

Wakati akitoa ombi la kugeuza kesi hiyo kuwa ya kinyumbani kupitia kwa wakili wake, mtoto huyo alikariri majuto yake kuhusu tukio hilo la kusikitisha.

“Tumepokea maombi ya wakili wa mshtakiwa, akiomba tupeleke shauri hilo kwenye suluhu ya kinyumbani. Hatupingi ombi hilo, lakini tutahitaji muda zaidi kuchanganua kesi kabla ya kuripoti tena kwa mahakama hii,” wakili wa serikali aliambia mahakama kulingana na jarida hilo.

Hati za mahakama zinaonyesha kuwa mshtakiwa alimuua mpwa wake usiku wa Agosti 28, 2022 katika kijiji cha Moiben katika kaunti ndogo ya Moiben.