Eldoret: Mshukiwa amuomba hakimu kumnunulia ugali kabla ya kumsomea mashtaka

Japheth Olindo alisema tangu ashikwe hajala chakula chake pendwa na kuwa hangeweza kufuatia mashtaka dhidi yake bila kula ugali.

Muhtasari

• Olindo pia alimtaka hakimu kumpa dhamana ya elfu 2 kwani angeendelea kuzuiliwa wahuni wangemchukua mke wake.

Mahakama
Mahakama
Image: MAHAKAMA

Mlinzi aliyetiwa mbaroni kwa tuhuma za kumshambulia mtu alizua kicheko katika mahakama ya Eldoret aliposema kwamba hangeweza kufuatilia mashtaka dhidi yake pasi na kupatiwa ugali.

Japhet Olindo alifikishwa mahakamani na kabla ya kuanza kusomewa mashtaka dhidi yake, alimuomba hakimu Keynes Odhiambo kumnunulia ugali mwanzo kabla ya shughuli yoyote kung’oa nanga.

Mshukiwa huyo alidai kwamba alikuwa katika hali mbaya karibu kuzimia kwa kile alitaja kwamba hakuwa amekula ugali – chakula chake pendwa tangu kuwekwa kizuizini.

Alimuomba hakimu kumfanyia mpango wa chakula hicho kwani bila hivyo hangeweza kuwa na umakini wa kufuatilia kesi dhidi yake mahakamani.

Hata hivyo, hakimu alimpa hakikisho la kuvumilia asomewe mashtaka na baadae amnunulie chakula hicho.

Kando na ombi la chakula, bwana Olindo pia aliomba hakimu kumpa adhabu ya chini na kumuachilia kwa dhamana ya elfu 2 kwa kile alisema kwamab angekaa jela kwa muda mrefu Zaidi, wahuni wangevamia boma lake nyumbani na kumnyakua mke wake.

Alikanusha mashtaka dhidi yake ya kuwashambulia watu watatu mnamo Machi 10 na kuachiwa kwa dhamana ya elfu 2 akisubiriwa kesi yake kutajwa tena mnamo Machi 16.