Sharon Otieno alidai nyumba ya milioni 25,kutambuliwa kama mke wa Obado-Shahidi

Pia alidai gari zuri kama mke wa Gavana na malipo ya Ksh.5 milioni kila mwezi.

Muhtasari
  • Shahidi, Lawrence Mule - aliyekuwa MCA - alikuwa kama mpatanishi kati ya Sharon na Obado.
  • Mule alieleza kuwa bosi huyo wa zamani wa Migori hakukana kuwa na uhusiano na Sharon, na kuongeza kuwa Obado alilalamikia maisha ya hali ya juu ambayo marehemu alikuwa akidai kutoka kwake.
Gavana Okoth Obado na mchepuko wake Sharon Otieno
Gavana Okoth Obado na mchepuko wake Sharon Otieno
Image: THE STAR

Marehemu Sharon Otieno alidai kutambuliwa kama mke wa aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado na kusisitiza kuishi viwango vya mke wa Gavana.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya awali Jumanne, shahidi aliambia mahakama kwamba Sharon alidai nyumba ya kukodisha ya kati ya Ksh.20 - 25 milioni, iwe Nairobi au Kisumu.

Pia alidai gari zuri kama mke wa Gavana na malipo ya Ksh.5 milioni kila mwezi.

Kwa ajili ya utunzaji wake kabla ya kuzaa, Sharon Otieno alidai Ksh.200,000, akisema kwamba lazima aende hospitali Nairobi kwa vile hali yake ilikuwa imebadilika.

"Nilijaribu kumshawishi aende hospitali ya Kaunti lakini alisema hawezi kwenda hospitali ya bei nafuu. Aliniambia (Mheshimiwa, kumbuka mimi ni mke wa gavana na nimembeba mtoto wa gavana)" aliambiwa.

Shahidi, Lawrence Mule - aliyekuwa MCA - alikuwa kama mpatanishi kati ya Sharon na Obado.

Mule alieleza kuwa bosi huyo wa zamani wa Migori hakukana kuwa na uhusiano na Sharon, na kuongeza kuwa Obado alilalamikia maisha ya hali ya juu ambayo marehemu alikuwa akidai kutoka kwake.

Mule alisema kuwa gavana alimpa Sharon dili la kumjengea nyumba yenye thamani ya Ksh.3-4 milioni na kumpatia nyumba hiyo. Dili ambalo Sharon alikubali.

“Tulikubaliana tutafute shamba linalogharimu takriban 800,000 ili gavana anunue kiwanja hicho na kumjengea nyumba,” Mule alieleza.

Hii ilipaswa kufanywa mnamo Agosti 2018.

Mule alisema kuwa kuna wakati walikutana na Oyamo pamoja na Sharon ambapo alipewa shilingi 200,000 kwa ajili ya huduma yake ya ujauzito na baada ya muda alimuomba aachane na jambo hilo.

Hata hivyo, baada ya kukutana na PA Michael Oyamo wa Obado, Sharon alisisitiza kwamba Mule aache mambo yake.

"Aliniambia atakutana na Oyamo huko Rongo ili kupata pesa za kumtunza, nikamwambia ni sawa."

Shahidi huyo aliweza kumtambua Oyamo ambaye alikuwa kortini lakini hakumkumbuka mtu ambaye Oyamo alikuwa akitembea naye wakati wa mkutano.

Mamake Sharon alikuwa atoe ushahidi wake leo lakini upande wa mashtaka ulisema hakuweza.