Paul Mackenzie na washukiwa wengine 28 kuzuiliwa kwa miezi 6 zaidi

Msaidizi wa DPP Jami Yamina alisema kipindi hicho kitawezesha polisi kuhitimisha uchunguzi wa vifo vya Shakahola.

Muhtasari
  • Mackenzie amekuwa chini ya ulinzi wa polisi kwa miezi mitano sasa, akikabiliwa na makosa yasiyopungua 12 yakiwemo ugaidi, mauaji, ushauri na kusaidia kujiua.
Mchungaji Paul Mackenzie

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma amewasilisha ombi jipya la kutaka mahakama iamuru kuzuiliwa kwa Paul Mackenzie na washtakiwa wenzake kwa miezi sita.

Msaidizi wa DPP Jami Yamina alisema kipindi hicho kitawezesha polisi kuhitimisha uchunguzi wa vifo vya Shakahola.

"Uchunguzi umesalia kuwa haujakamilika baada ya kutokamilika kwa amri ya awali ya mahakama iliyoelekeza kuzuiliwa zaidi kwa Mackenzie na washtakiwa wenzake kwa siku 47," alisema.

Katika ombi hilo, DPP alisema wataalamu wa magonjwa wa serikali wanahitaji angalau miezi sita ya ziada kukamilisha mchakato wa kuchambua DNA ili kubaini kwa ukamilifu utambulisho wa kweli wa miili iliyofukuliwa.

"Uchambuzi wa DNA wa miili 429 iliyotolewa katika msitu wa Shakahola ni dhaifu, wa gharama, mgumu, na unatumia muda," Yamina alisema.

Kesi hiyo itatajwa Oktoba 12, 2023.

Mackenzie amekuwa chini ya ulinzi wa polisi kwa miezi mitano sasa, akikabiliwa na makosa yasiyopungua 12 yakiwemo ugaidi, mauaji, ushauri na kusaidia kujiua.

Nyingine ni; utekaji nyara, itikadi kali, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya ubinadamu, ukatili wa watoto, ulaghai na utakatishaji fedha.

Mnamo Juni 2, baada ya kuisha kwa siku 30 za awali, DPP na DCI waliomba kuongezwa kwa amri za ulezi kwa siku nyingine 60.

Kabla ya mahakama kutoa uamuzi kuhusu ombi hilo jipya, Mackenzie na washtakiwa wenzake waligoma kula kwa siku 10 wakiwa kizuizini.