Rais Ruto asisitiza kuwa mpango wa nyumba za bei nafuu utaendelea licha ya uamuzi wa mahakama ya rufaa

"Walipaswa kutupa nafasi ya kukamilisha sheria lakini tunaenda kukamilisha sheria na tunaenda kuikamilisha."

Muhtasari

• Ruto alisema mradi huo kwa sasa unaajiri zaidi ya vijana 130,000 na idadi hiyo itakuwa imepanda hadi 300,000.

Rais William Ruto
Rais William Ruto
Image: Twiter

Rais William Ruto amesisitiza kuwa mpango wa kuhakikisha Wakenya wote wana nyumba za bei nafuu na zinazostahili utaendelea. 

Akizungumza katika soko la Kangeta eneo la Igembe, Ruto alisema tayari serikali inaunda sheria itakayoongoza mradi wake wa ujenzi wa nyumba. Alisisitiza kuwa mahakama ilipaswa kuwaruhusu kukamilisha kuunda sheria. 

Rais aliongeza kuwa licha ya uamuzi huo, atasonga mbele na mpango huo ambao umetoa fursa kwa vijana, akisisitiza kwamba hapo ndipo maslahi ya umma yalipo. 

“Nataka niseme ili kuepusha mashaka tayari tunatunga sheria ambayo mahakama iliidhinisha twende tukaitunge, walipaswa kutupa nafasi ya kukamilisha sheria lakini tunaenda kukamilisha sheria na tunaenda kuikamilisha. Tutasonga mbele kwa kuhakikisha tunaunda nafasi za kazi kwa vijana wa nchi yetu kwa sababu ndivyo watu wa Kenya wanataka. Hilo ndilo jambo sahihi na hapo ndipo maslahi ya umma yalipo," Ruto alisema Jumanne. 

Rais aliwakashifu waliokwenda kortini kusitisha mchakato huo akisema kuwa wanaishi maisha bora na watoto wao ilhali hawataki vijana wasio na kazi wapate maisha bora kupitia mradi wa Makazi.

Ruto alisema mradi huo kwa sasa unaajiri zaidi ya vijana 130,000 na idadi hiyo itakuwa imepanda hadi 300,000.

 "Mpango wa nyumba utatupatia ajira katika viwanda vya kutengeneza saruji na chuma. Utahakikisha wahandisi, waashi na maseremala wanapata ajira," alisema. 

"Nataka kuwaambia watu ambao wamekwenda mahakamani, wengi wao wana kazi, wanataka kuwanyima fursa watu ambao hawajawahi kufanya kazi. Tuko kwenye dhamira ya kuhakikisha usawa kwa watu wote wa Kenya." 

Matamshi yake yanajiri baada ya Mahakama ya Rufaa siku ya Ijumaa kukataa kusitisha amri zinazozuia serikali kukata ushuru wa nyumba kutoka kwa Wakenya.

Majaji Lydia Achode, John Mativo na Gatembu Kairu katika kukataa ombi la serikali, walisema maslahi ya umma yapo katika kusubiri uamuzi wa rufaa hiyo. Kwa hivyo, hii inamaanisha kuwa ushuru wa nyumba unabaki kusimamishwa kama ilivyoamuliwa na Mahakama Kuu. 

Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Hazina ya Kitaifa walikuwa wamekata rufaa baada ya Mahakama Kuu kupata makato hayo kuwa kinyume na katiba.