Wawili wapigwa faini ya milioni 40 baada ya kupatikana na ngozi za nyoka na za mamba

Mahakama iliamuru kuwa washtakiwa watatumikia kifungo cha miaka 10 iwapo watashindwa kulipa faini hiyo.

Muhtasari

•2 walihukumiwa kulipa faini ya Ksh 20milioni kila mmoja kwa kosa la kupatikana na ngozi saba za chatu na ngozi mbili za mamba.

•Washukiwa walipatikana na ngozi za chatu na za mamba katika Soko la Ndalani-Sofia ndani ya Kaunti ya Machakos mnamo Novemba 27, 2019.

Nyoka
Image: BBC

Wanaume wawili mnamo siku ya Jumatano walihukumiwa kulipa faini ya Ksh 20milioni kila mmoja kwa kosa la kupatikana na ngozi saba za chatu na ngozi mbili za mamba.

Mahakama ya Kithimani katika kaunti ya Machakos iliamuru kuwa Oscar Kambona Musyimi na Anthony Mutie watatumikia kifungo cha miaka 10 iwapo watashindwa kulipa faini hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, washtakiwa hao walikuwa wameshtakiwa kwa kosa la kumiliki mali za wanyamapori kinyume na kifungu cha 92 cha sheria ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori, namba 47 ya mwaka 2013.

Hii ni baada ya washukiwa kupatikana na ngozi hizo za chatu na za mamba katika Soko la Ndalani-Sofia ndani ya Kaunti ya Machakos mnamo Novemba 27, 2019.

“Wakati akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi Mhe. Paul Wechuli aliona kwamba mashahidi wote 6 wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi wao walitoa ushahidi thabiti na shirikishi ambao washtakiwa walishindwa kuutikisa wakati wa kuhojiwa,” ilisema taarifa ya DPP.

Kesi hiyo iliyochukua muda wa miaka minne iliendeshwa na Fredrick Nderitu Kimathi, DPP amesema.