Washukiwa wa mlipuko wa gesi nchini Kenya kuzuiliwa kwa Siku 21

Muhtasari

• Polisi wanasema kuwa wanachunguza mauaji, njama ya kutenda uhalifu, vitendo vya uzembe, kusababisha madhara na matumizi mabaya ya ofisi zao dhidi ya washukiwa.

Image: BBC

Washukiwa wanne waliokamatwa kuhusiana na tukio la mlipuko wa gesi ambao hadi sasa umesababisha vifo vya watu saba wataendelea kuzuiliwa na polisi kwa 21 ili kuruhusu uchunguzi kukamilika.

Washukiwa hao ni pamoja na Derrick Kimathi, ambaye alikuwa mmiliki wa kiwanda cha gesi , Joseph Makau, David Walunya Ong'are na Marrian Mutete Kioko ambao ni maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA).

Polisi wanasema kuwa wanachunguza mauaji, njama ya kutenda uhalifu, vitendo vya uzembe, kusababisha madhara na matumizi mabaya ya ofisi zao dhidi ya washukiwa.

Walifikishwa kortini kwa mara ya kwanza Jumanne mbele ya hakimu wa Nairobi Dolphina Alego ambapo wapelelezi waliwasilisha ombi tofauti la kuwazuilia kwa siku 21.

Kimathi ndiye mmiliki wa kiwanda haramu cha kujaza gesi eneo la Mradi, Embakasi Mashariki ambapo moto ulizuka Alhamisi usiku na kuua watu saba na kuwajeruhi karibu wengine 300.

Upande wa mashtaka uliiambia mahakama kuwa watu hao wanne walikuwa wamejificha tangu kuripotiwa kwa kesi hiyo na rasilimali nyingi zimetumika kuwasaka, na kuongeza kuwa hawapaswi kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu .