Upande wa mashtaka wataka Kang’ethe kupelekwa gereza la Viwandani

Kang’ethe alikamatwa Jumanne usiku huko Ngong baada ya kutoroka polisi katika kituo cha Muthaiga

Muhtasari

• Kang’ethe ataruhusiwa kuwasiliana na mawakili wake pekee na wala sio wakili mwingine.

Kevin Kang'ethe alifikishwa tena katika Mahakama ya Milimani baada ya kukamatwa kutoka kwa maficho yake huko Ngong mnamo Februari 14, 2024. Picha: DOUGLAS OKIDDY
Kevin Kang'ethe alifikishwa tena katika Mahakama ya Milimani baada ya kukamatwa kutoka kwa maficho yake huko Ngong mnamo Februari 14, 2024. Picha: DOUGLAS OKIDDY

Upande wa mashtaka umeitaka mahakama kumshikilia mshukiwa wa mauaji Kevin Kang’ethe Kinyanjui katika gereza la Viwandani kwasababu kuna hatari ya yeye kutoroka tena kutoka korokoro za polisi.

Kang’ethe, ambaye anasakwa nchini Marekani kwa mauaji ya mwanamke, alikamatwa Jumanne usiku huko Ngong baada ya kutoroka mikononi mwa polisi katika kituo cha Muthaiga mnamo Februari 7, 2024.

Akiwa mbele ya Hakimu wa mahakama ya Milimani Lucas Onyina, mwendesha mashtaka Vincent Monda aliambia mahakama kuwa iwapo ombi hilo litakubaliwa, Kang’ethe ataruhusiwa kuwasiliana na mawakili wake pekee na wala sio wakili mwingine.

Vile vile, mahakama ilihimizwa kuamuru kwamba mawakili hao wanapomtembelea ni lazima waambatane na mpelelezi.Mahakama iliambiwa kwamba ikiwa atahitaji matibabu yoyote inapaswa kufanywa kwa kushauriana na madaktari wa serikali walio katika gereza la Industrial area.

Hata hivyo, Kang’ethe kupitia kwa mawakili wake alipinga ombi hilo, akisema hakuna shtaka lililowasilishwa dhidi yake, na ombi dhidi yake mahakamani ni la kurejeshwa Marekani.

"Iwapo lolote lingetokea basi ni juu ya serikali kuweka sawa nyumba yake. Ikiwa hawezi kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga basi kuna vituo vingine vingi nchini," wakili wa Kang'ethe aliwasilisha.

Kang’ethe alikamatwa katika eneo la Parklands mnamo Januari 29, baada ya amri kutoka kwa Marekani.

Anadaiwa kumuua Margaret Mbitu huko Massachusetts mnamo Oktoba 31, 2023 kwa kumchoma visu vingi usoni na shingoni kabla ya kuuacha mwili wake kwenye gari lililokuwa limefungwa kwenye karakana ya kuegesha magari Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Boston Logan.