Jinsi Jowie Irungu anaweza kujinusuru dhidi ya hukumu ya kifo

Jaji Grace Nzioka aliamuru kwamba Jowie amehukumiwa kunyongwa kwa mauaji ya mfanyibiashara Monica Kimani.

Muhtasari

•Jaji Grace Nzioka alitoa hukumu ya kifo dhidi ya Jowie katika Mahakama ya Milimani siku ya Jumatano alasiri.

•Wakati akitoa hukumu, Jaji Grace Nzioka alibainisha kuwa mshtakiwa hana sifa ya kutumikia kifungo cha nje.

mbele ya Hakimu Grace Nzioka aliyehukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani, katika Mahakama ya Milimani mnamo Machi 13, 2024.
Jowie Irungu, mbele ya Hakimu Grace Nzioka aliyehukumiwa kifo baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani, katika Mahakama ya Milimani mnamo Machi 13, 2024.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Joseph ‘Jowie’ Irungu bado ana fursa ya kujinusuru dhidi ya hukumu ya kunyongwa.

Mfungwa huyo sasa ana siku kumi na nne baada ya kuhukumiwa za kuwasilisha rufaa dhidi ya hukumu ya kifo ambayo alipewa siku ya Jumatano. 

Jaji Grace Nzioka alitoa hukumu hiyo katika Mahakama ya Milimani siku ya Jumatano alasiri kufuatia hukumu ya hatia iliyotolewa mnamo Februari 9, 2024. Mtuhumiwa alipatikana na hatia ya kumuua mfanyibiashara Monica Kimani mnamo Septemba 2018.

Wakati akitoa hukumu, Jaji Grace Nzioka alibainisha kuwa mshtakiwa hana sifa ya kutumikia kifungo cha nje.

“Kwa kuzingatia yote nimesema, kwa hivyo, ninaamuru kwamba mshtakiwa wa kwanza Joseph Kuria Irungu almaarufu Jowie amehukumiwa kunyongwa kama ilivyoelezwa kwa kosa la mauaji chini ya kifungu cha 204 cha kanuni ya adhabu ya Kenya isipokuwa hukumu hiyo itolewe kando na mahakama yenye mamlaka," Jaji Nzioka alisema.

Hukumu hiyo ilitolewa baada ya mahakama kumpata Jowie na hatia ya mauaji ya Monica Kimani.

Mahakama iligundua kuwa mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 28 hakufa kifo cha kawaida, bali aliuawa kama ilivyothibitishwa na upande wa mashtaka.

Hukumu ya Jowie jela inamaliza kesi ya mauaji ambayo imekuwa ikiendelea kwa miaka sita iliyopita.

Hukumu hiyo ilikusudiwa kutolewa Machi 8, 2024 lakini ikaahirishwa hadi Jumatano, Machi 13 baada ya mawakili wa Jowie kuwasilisha stakabadhi muhimu wakiwa wamechelewa.

Endapo mfungwa atawasilisha rufaa na kufanikiwa, shtaka lake linaweza kupunguzwa au kuondolewa kulingana na ushahidi atakaotoa dhidi ya hukumu hiyo.

Aliyekuwa mtangazaji wa televisheni Jacque Maribe, ambaye alishtakiwa pamoja na Jowie hapo awali, aliondolewa mashtaka ya mauaji.

Nzioka alisema shtaka la mauaji sio shtaka sahihi ambalo upande wa mashtaka ungependelea dhidi yake.

Alisema upande wa mashtaka haukumweka Maribe katika eneo la uhalifu.