Tiktoker ahukumiwa kifungo cha miaka 6 jela kwa kumtusi Rais Museveni na familia yake

Alishtakiwa kwa kuchapisha video kwenye TikTok ambapo alitoa maoni machafu na ya kudhalilisha kuhusu Mkuu wa Nchi, mkewe Janet na Mwanawe wa Kwanza, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.

Muhtasari

• Mkazi wa Nama, wilayani Mukono, Awebwa alikamatwa wiki iliyopita na kufikishwa mahakamani ambapo alikiri mashitaka yote manne aliyosomewa.

• Hakimu Mashauri alimhukumu Awebwa miaka sita kwa kila kosa. Hata hivyo, atatumikia vifungo vyote vinne kwa wakati mmoja.

 

MSHUKIWA
MSHUKIWA
Image: HISANI

TikToker mmoja katika taifa jirani la Uganda amejipata pabaya baada ya kujirekodi video na kupakia kwenye mtandao huo wa video akimtupia rais Yoweri Museveni matusi ya nguoni pamoja na familia yake.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka nchini humo, kijana huyo wa umri wa tineja alihukumiwa Jumatano jela kifungo cha miaka 6 kwa kumkosea heshima mkuu wa nchi na familia yake.

Edward Awebwa alihukumiwa kwa ombi lake mwenyewe la hatia, na Hakimu Mfawidhi wa daraja la kwanza wa Mukono Stella-Maris Amabirisi.

Alishtakiwa kwa kuchapisha video kwenye TikTok ambapo alitoa maoni machafu na ya kudhalilisha kuhusu Mkuu wa Nchi, mkewe Janet na Mwanawe wa Kwanza, Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye pia ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya UPDF.

Mkazi wa Nama, wilayani Mukono, Awebwa alikamatwa wiki iliyopita na kufikishwa mahakamani ambapo alikiri mashitaka yote manne aliyosomewa.

Hakimu Mashauri alimhukumu Awebwa miaka sita kwa kila kosa. Hata hivyo, atatumikia vifungo vyote vinne kwa wakati mmoja.

Hakimu katika uamuzi wake, alisema hakumpa mshukiwa adhabu ya juu zaidi kwa sababu ya umri wake mdogo na ukweli kwamba haukupoteza muda wa mahakama kwa kupeleka kesi mahakamani.

Upande wa mashitaka wa serikali ukiongozwa na Janet Kitumbo ulikuwa umeomba adhabu hiyo iwe ya juu zaidi ili iwe kizuizi kwa vijana wengine wanaoendelea kutumia vibaya mitandao ya kijamii.