Mshukiwa mwingine wa kisa ambapo mwanablogu kutoka mkoa wa
Pwani alitekwa nyara na kulawitiwa amefikishwa mbele ya hakimu Robert Mbogo
katika mahakama ya Shanzu jijini Mombasa na kukana madai dhidi yake.
Mshukiwa huyo alikamatwa katika eneo la Lunga Lunga karibu
na mpaka wa Kenya na Tanzania baada ya uchunguzi wa maafisa wa usalama kufanywa.
Mshukiwa amesomewa mashtaka manne yanayohusiana na ukatili
uliofanyiwa mwanablogu aliyeathirika ikiwemo shtaka la kupanga njama ya kutenda
uhalifu na utekaji nyara akiwa na nia ya kumzuilia mwathiriwa.
Katika ushahidi uliowasilishwa mahakamani, upande wa
mashtaka umesema kwamba mshukiwa huyo alishirikiana na washukiwa wengine wanne
katika kumteka nyara mwanablogu.
Mbali na kuhusika katika kitendo cha utekaji nyara, hakimu
Robert Mbogo alielezwa kuwa mshukiwa alimvamia mwathiriwa kwa kumpiga mateke na
ngumi kitendo ambacho kilisababisha majeraha kwa mwanablogu ambaye alitekwa
nyara.
Akiwa mbele ya mahakama ya Shanzu, mshukiwa alikana madai
aliyosomewa na hakimu kuamuru kuzuziliwa kwake katika rumande ya Shimo La Tewa
akisubiri kufanya maombi ya dhamana mnamo Ijumaa Novemba 15.
Washukiwa wa kwanza wane walifikishwa mahakamani humo wiki
sita zilizopita na kushtakiwa kwa hatia ya utekaji nyara na kulawiti
mwanablogu.
Washukiwa wote watano ambao wamefikishwa mahakamani wakiwemo
wanawake wawili wlikana mashtaka dhidi yao.