Mahakama ya Kahawa mnamo Jumanne, ilibaini kuwa maafisa wakuu 12 wa jela ya Kamiti wana kesi ya kujibu kuhusu kutoroka kwa washukiwa watatu katika gereza la Kamiti mnamo Novemba 14, 2021.
Kumi na wawili hao, walishtakiwa na hatia ya kupuuza majukumu yao rasmi na kusaidia wafungwa wa ugaidi kutoroka gerezani.
Mahakama ya Kahawa iliamuru kuwa kesi iliyowasilishwa na upande wa mashtaka ukiongozwa na James Machirah, Ken Amwayi, Harrison Kiarie na Gideon Kiprono ilikuwa na uzito wakutosha kwa washukiwa kujitetea dhidi ya kesi hiyo.
Maafisa hao wa magereza wanashukiwa kuwasaidia wafungwa waliopatikana na hatia ya ugaidi kuhepa jela licha ya mahakama kuwahukumu vifungo mbali mbali jela. Washukiwa waliotoroka na kisha kukamatwa tena ni Musharraf Abdalla, Mohame Ali na Joseph Juma ambao wanahudumia vifungo vya miaka 42, 22 na 15 mtawalia gerezani.
Aidha mmoja wa maafisa hao anakabiliwa na kesi nyingine tofauti na wengine ambapo anadaiwa kuwa aliitisha mkutano wa kuwasaidia magaidi kuotoka jela. Mahakama ilielezwa kuwa afisa huyo, afisa huyo anadaiwa kuwezesha kuondolewa kwa magaidi hao kutoka seli nambari 2 hadi seli nambari 6 kabla ya magaidi hao kutoroka jela.
Kesi dhidi wa 12 hao itasomwa tena mwakani mwezi Januari
tarehe 13 ambapo mahakama itatoa mwelekeo zaidi.