Mahakama Kuu imeamuru serikali kutoa ushahidi kuthibitisha madai kuwa mkataba wa Adani-JKIA umeghairiwa.
Jaji Bahati Mwamuye alitoa agizo hilo baada ya Wakili Ezra Makori anayewakilisha Adani Group kusema wangependa kuachiliwa kutokana na kesi hiyo kwa vile miradi hiyo imefutwa.
Hata hivyo, Tony Gachoka na wanasheria wa Mlima Kenya waliowasilisha maombi katika kesi hiyo walisema hakuna ushahidi kwamba agizo la Rais William Ruto la kughairi kandarasi hiyo limefanyika.
Walalamishi hao walisema lazima kuwe na uwajibikaji kwa walioanzisha mradi uliopingwa kabla ya suala hilo kutafutwa.
"Kesi ya maslahi ya umma kama hii lazima iendelee pale ambapo utata umeibuka kuhusiana na mali ya kukodisha ni ya Wakenya," walisema.
Kibe alisisitiza kuwa suala hilo linafaa kuendelea kwa hitimisho lake la kimantiki kwani pia wanapinga uhalali wa vifungu mbalimbali katika Sheria ya PPP ambayo mkataba wa Adani-JKIA uliasisiwa.
"Tunazungumza kuhusu ufisadi wa hali ya juu. Tunahitaji kujua ni nini hasa kilighairiwa," alisema Kalonzo.
Mwamuye huku akiitaka serikali kutoa ushahidi kuwa makubaliano hayo kufikia sasa yamefutiliwa mbali pia alitoa agizo la kumzuia Adani na chombo kingine chochote kuchukua JKIA hadi kuamuliwa kwa kesi iliyo mahakamani.