Sudi yupo Eldoret, sio Uturuki- Mahakama yatambua

Muhtasari

•Sudi alikosa kufika kusikizwa kwa kesi yake ya ulaghai siku ya Jumatano, akidai alikuwa amesafiri hadi Uturuki kutafuta matibabu.

•Mahakama iliahirisha kesi hiyo Jumatano ili kuipa timu ya utetezi muda wa kutoa ushahidi thabiti unaothibitisha mteja wao yuko Uturuki.

Oscar Sudi
Oscar Sudi
Image: MAKTABA

Mahakama imebaini kuwa mbunge wa Kapsaret Oscar Sudi yuko mjini  Eldoret kinyume na ripoti kwamba yupo nje ya nchi.

Sudi alikosa kufika kusikizwa kwa kesi yake ya ulaghai siku ya Jumatano, akidai alikuwa amesafiri hadi Uturuki kutafuta matibabu.

Haikuwekwa wazi mahakamani ugonjwa ambao mbunge huyo anaugua.Lakini siku ya Alhamisi mahakama ilibaini kuwa mbunge huyo bado yuko nchini.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo Jumatano ili kuipa timu ya utetezi muda wa kutoa ushahidi thabiti unaothibitisha mteja wao yuko Uturuki.

Lakini Hakimu Felix Kombo bado hakuridhika na hati zilizotolewa na timu ya wanasheria wa Sudi.

“Hati hizi bado hazionyeshi anuani maalum ya mahali hospitali ilipo,” Kombo alisema.

“Pia sasa ni wazi kuwa mteja wako hakusafiri, kwanini ulisema alisafiri, kama alikupa maelekezo ambayo si ya kweli niambie na uiachie mahakama,” alisema Kombo.

Mahakama pia ilikabiliana na hati ya matibabu iliyotiwa saini na mmoja, Austin Okoth.

"Je Austin Okoth ni daktari?" Kombo alisema.

"Siwezi kuthibitisha kwa mamlaka kwa sababu hizi zilikuwa nyaraka nilizotumwa na mteja wangu," mmoja wa mawakili wa Sudi alisema.

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo kwa ufupi ili kutoa nafasi kwa upande wa utetezi kupanga mambo yao.

Walisema Okoth ni daktari na hawakuwa na tatizo na hilo kuthibitishwa.

Baadaye Kombo aliagiza kesi iendelee kusikilizwa bila kuwepo Sudi. Mawakili wake hawakupinga vivyo hivyo.