Kalonzo akana madai kuwa wanachama wa OKA wanashurutishwa kuunga Raila mkono, asema atakuwa debeni mwaka ujao

Kalonzo amesema kuwa bado hajatangaza rasmi kuwa atagombea kiti cha urais kwani bado hajapatiwa kibali na chama chake cha Wiper pamoja na muungano wa OKA

Muhtasari

•Kalonzo amesema kuwa  amefanya uamuzi wa kuwa kwenye debe mwaka ujao ila bado anashaurina na timu yake ili kujua mwelekeo atakaochukua.

•Mgombeaji huyo wa urais kwenye chaguzi za 2017 amesema kuwa timu yake ya OKA kwa sasa inajiandaa na kilichosalia kwa sasa ni kujua mpangilio wa uongozi.

Kalonzo Musyoka katika studio za Radio Jambo mnamo tarehe 1 mwezi Septemba
Kalonzo Musyoka katika studio za Radio Jambo mnamo tarehe 1 mwezi Septemba
Image: ANDREW KASUKU

Kiongozi wa Wiper Stephen Kalonzo Musyoka amesema kuwa yuko tayari kuchukua uongozi wa nchi ya Kenya mwaka ujao.

Akiwa kwenye mahojiano na Gidi katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi, Kalonzo amesema kuwa  amefanya uamuzi wa kuwa kwenye debe mwaka ujao ila bado anashaurina na timu yake ili kujua mwelekeo atakaochukua.

Kalonzo amesema kuwa bado hajatangaza rasmi  kuwa atagombea kiti cha urais kwani bado hajapatiwa kibali na chama chake cha Wiper pamoja na muungano wa OKA. .

"Bado tutafanya matamshi rasmi wakati unaofaa kabla ya mwezi rasmi. Uamuzi wengi wamefanya lakini lazima tujiandae. Lazima nipatiwe kibali na chama changu  cha Wiper na  wenzangu wa OKA" Kalonzo amesema.

Mgombeaji huyo wa urais kwenye chaguzi za 2017 amesema kuwa timu yake ya OKA kwa sasa inajiandaa na kilichosalia kwa sasa ni kujua mpangilio wa uongozi.

Amesema kuwa janga la Corona limeathiri mipango yao na kuchangia katika kuchelewa hatua yao ya kukutana na wananchi ila wanajiandaa.

Kalonzo alieleza imani yake kuwa Wakenya wengi wanampendekeza kuchukua nafasi hiyo mwaka ujao..

Kalonzo pia amepuuzilia mbali madai kuwa wanachama wa Wiper wanashurutishwa kumuunga mkono kinara wa ODM Raila Odinga kwenye azma yake kuwania kiti cha urais mwaka ujao.

"Hakuna mambo ya kushurutishwa. Sisi ni viongozi shupavu na wakakamavu.Vikao vya rais sio kwa sababu ya kushurutisha watu, ni kawaida kwa kila demokrasia kwa aliye madarakani kushauriana na viongozi wengine. Mashauriano hayo yasionekane kama ni mambo ya kushurutishwa" Kalonzo aliambia Gidi.

Alisema kuwa muungano wa OKA utatoa taarifa rasmi wakati utakaofaa.

Kalonzo alisema kuwa ana imani OKA itapata ushindi mkubwa dhidi ya naibu rais William Ruto na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.

"Mheshimiwa Raila Odinga na mheshimiwa William Ruto tunawajua sana. Sisi tutawabwaga raundi ya kwanza" Amesema Kalonzo.