logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mpango wa 'Dishi na County' umeongeza idadi ya watoto shuleni- Gavana Sakaja

Sakaja alisema wamekamilisha ujenzi wa majiko kadhaa  ambayo tayari yanahudumia watoto zaidi ya 80,000.

image
na Samuel Maina

Habari01 September 2023 - 07:22

Muhtasari


  • •Gavana Sakaja alisema kuwa wameona watoto ambao walikuwa hawaendi shuleni wakianza kuhudhuria masomo.
  • •Gavana huyo wa UDA pia aliweka wazi kuwa mpango huo umepunguza msongo wa mawazo kwa wazazi kwa kiwango kikubwa.

Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja amebainisha kuwa mpango wa kuwalisha watoto shuleni wa ‘Dishi na County’ umesaidia kuongeza idadi ya watoto wanaokwenda shule.

Akizungumza wakati wa mahojiano na Radio Jambo Ijumaa asubuhi, Sakaja alisema kuwa wameona watoto ambao walikuwa hawaendi shuleni wakianza kuhudhuria masomo.

Alisema kuwa mpango wa ulishaji chakula umewaondoa watoto kutoka majumbani mwao na sasa wanajipeleka wenyewe shuleni.

“Pale tulianzisha Dagoretti Kusini, usajili wa watoto kwenye mpango ulipanda juu kwa 150%. Wale watoto walikuwa hawaendi shule sasa wanajileta wenyewe. Ni njia ya kuwavutia shuleni,” Sakaja alisema.

Gavana huyo wa UDA pia aliweka wazi kuwa mpango huo umepunguza msongo wa mawazo kwa wazazi kwa kiwango kikubwa.

“Unapata kuna husla anaenda mjengo hajui kama atapata ama hatapata, lakini anajua apate ama asipate, mtoto wake lazima akule. Inapunguza stress nyingi sana, watu wanafurahia,” alisema.

Kuongezea, alisema kuwa mpango wa lishe wa ‘Dishi na County’ umetoa ajira kwa wazazi wapatao 1,500 kutoka kaunti ya Nairobi.

"Inatengeneza ajira kwa dereva, wapishi, wale wakugawa chakula na kusafisha," alisema.

Alibainisha kuwa wazazi kuajiriwa jikoni kuwapikia watoto ni hatua nzuri kwani wanakuwa waangalifu zaidi kwani hawataki kuwatilia sumu watoto wao.

Sakaja alisema kuwa awali walikuwa wanalenga kutoa chakula kwa watoto 250,000 jijini Nairobi lakini kulingana na mwitikio wa uandikishaji kwenye programu hiyo, wamechochewa kuongeza lengo hadi watoto 350,000.

Mkuu huyo wa kaunti alifichua kuwa tayari wamekamilisha ujenzi wa majiko kadhaa katika maeneo fulani ya Nairobi ambayo tayari yanahudumia watoto zaidi ya 80,000. Alisema pamoja na washirika wao, wanalenga kujenga jikoni takriban 14.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved