logo

NOW ON AIR

Listen in Live

"Mwenye pesa sijui anakaa vipi" Mfanyibiashara Anne Njeri afunguka kuhusu umiliki wa mafuta ya Sh17 bilioni

Bi Anne Njeri aliibua kauli za kejeli kwa watu wenye shaka kuhusu jinsi tajiri anavyoonekana.

image
na SAMUEL MAINA

Habari20 November 2023 - 05:43

Muhtasari


  • •Anne Njeri ameshangaa ni kwa nini idadi kubwa ya Wakenya wanatilia shaka uwezo wake wa kuagiza mafuta ya thamani ya Ksh17bilioni.
  • •Mfanyibiashara huyo alithibitisha kuwa mamake hajui utajiri wake licha ya kwamba anajua kuwa anafanya biashara.
Mfanyabiashara Anne Njeri Njoroge akizungumza katika mahakama kuu mjini Mombasa mnamo Novemba 14, 2023

Mfanyibiashara Anne Njeri Njoroge ameshangaa ni kwa nini idadi kubwa ya Wakenya wanatilia shaka uwezo wake wa kuagiza mafuta ya thamani ya Ksh17bilioni ambayo imeshikiliwa katika bandari ya Mombasa kwa zaidi ya mwezi.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Citizen TV katika eneo lililofichika, mfanyibiashara huyo ambaye amekuwa akitamba kwa wiki chache zilizopita aliibua kauli za kejeli kwa watu wenye shaka kuhusu jinsi tajiri anavyoonekana.

“Mwenye pesa sijui ana sura gani. Mwenye pesa sijui anakaa kivipi. Mwenye pesa, hajitambui. Mwenye pesa sijui anakaa sura gani,” Anne Njeri alisema.

Mfanyibiashara huyo mwenye utata alisema iwe tajiri au maskini, kila mtu anaonekana kama binadamu na hakuna tofauti ya wazi.

Bi Anne Njeri alikuwa akijibu maswali mengi yaliyoibuliwa na Wakenya kuhusu uwezo wake wa kumiliki kiasi kikubwa cha mafuta yenye thamani ya mabilioni ya pesa. Kundi kubwa la Wakenya limekuwa likitilia shaka utajiri wake na kudai kwamba yeye haonekani kama mtu aliye na uwezo wa kuagiza kiasi hicho cha mafuta. Baadhi wamedai kuwa mafuta hayo ni ya bilionea mashuhuri wa Kenya, pengine mwanasiasa na kwamba Anne Njeri anatumiwa tu kuficha utambulisho wa mtu fulani.

Katika mahojiano hayo hayo, mfanyibiashara huyo alithibitisha kuwa mamake hajui utajiri wake licha ya kwamba anajua kuwa anafanya biashara.

“Mama hajui pesa zangu ziko kiasi gani. Anajua mimi ni mfanyibiashara. hiyo anajua. Lakini unajua mambo mengi sio ya kusema,” alisema.

Wiki jana, mamake Anne Njeri alihojiwa na wanahabari ambapo alikiri kwamba hakuwahi kujua kwamba bintiye ni tajiri kiasi hicho.

Bi Pauline Njoroge alisema kwamba kando na kutojua utajiri wa bintiye, pia hajawahi kutana naye kwa kipindi cha miaka 5 iliyopita.

“Ni ukweli ninamkosa sana binti yangu, lakini ninataka aje kuniona, lakini kila mara ananiambia kwamba yuko bize,” mama huyo wa miaka 71 aliambia NTV.

“Huwa tu tunaonana kupitia kwa video na nimekubali hilo kwa sababu kama ako sawa pia mimi ninafarijika,” aliongeza.

Bi Anne Njeri ambaye anadaiwa kuwa mmiliki wa mafuta ya thamani ya Ksh17bilioni ambayo yameshikiliwa katika bandari ya Mombasa kwa zaidi ya mwezi amekuwa akivuma wiki chache zilizopita na anatarajiwa kujiwasilisha katika ofisi za Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai, jini Nairobi wiki hii.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved