Ghost azungumzia maisha yake; alama alizopata, kazi ya kwanza,mshahara wa kwanza...

Mtangazaji Jacob ‘Ghost’ Mulee amejibu baadhi ya maswali ya kibinafsi kumhusu.

Muhtasari

•Ghost amejibu baadhi ya maswali kumhusu kama vile alama alizopata katika shule ya upili, kazi  yake ya kwanza, chakula anachopenda, wakati anaopendelea zaidi katika siku, kazi ambayo angekuwa anafanya asingekuwa mtangazaji, miongoni mwa mengine.

Ghost Mulee studioni
Ghost Mulee studioni
Image: RADIO JAMBO

Mtangazaji tajika wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Jacob ‘Ghost’ Mulee amejibu baadhi ya maswali ya kibinafsi kumhusu.

Katika mahojiano ya wazi na mwanahabari Samuel Maina, kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alitoa maelezo ya ndani kumhusu kama vile alama alizopata katika shule ya upili, kazi yake ya kwanza, chakula anachopenda zaidi, wakati anaopendelea zaidi katika siku, kazi ambayo angekuwa anafanya kama asingekuwa mtangazaji, miongoni mwa mambo mengine.

Kuhusu chakula anachopenda zaidi, mtangazaji huyo mcheshi alisema anapenda kula ugali kwa samaki.

“Saa ingine napenda ugali kwa matumbo,” Ghost Mulee alisema.

Pia alifichua kuwa anapendelea kutumia wakati wake wa mapumziko na wanyama katika mbuga ya kitaifa akisema kuwa wanyama humpa mazingira mazuri ya kupumzika.

Pia alisema, tofauti na binadamu, wanyama wana fadhila bora kwa jinsi wanavyohusiana na wenzao.

"Ninapenda kwenda kwenye mbuga ya wanyama wakati wa mapumziko. Unajua hao wanyama wakati mwingi wanatulia, hawana stori mingi, hawana wivu. Wewe unawaona, Simba akiua mnyama mmoja, ni mmoja. Hataki kuua ndovu, mara aue Kifaru. Sisi binadamu hutaka kumiliki kila kitu. Kwa hiyo, wildife ndiyo maskani yangu ya kurelax,” alisema.

Ghost pia alidokeza kuwa anapendelea saa za asubuhi kuliko saa za jioni akieleza kuwa amezoea kuamka mapema sana.

“Mimi ni mtu wa asubuhi sana. Mimi ata kama sikuji kazi, saa zingine napatanga tu alarm imelia naamka. Unajua ukizoea inakuwa akilini mwako iko hivyo. Mimi ni mtu wa asubuhi, ikifika jioni nimeshamaliza,” alisema.

Pia alifichua kuwa kazi yake ya kwanza, alifanya kazi kama mfanyakazi wa kawaida ambapo angepata chini ya shilingi mia tano kwa wiki.

“Kazi yangu ya kwanza ilikuwa kibarua huko Kenya Airways, tulikuwa tunalipwa karibu 70 bob per day. Tulikuwa tunalipwa kila baada ya wiki mbili ama kila wiki. Kwa hiyo najua 70*7, ilikuwa napata karibu 490 kwa wiki,” Ghost alisema.

Aliongeza, “Wakati huo 70 ilikuwa pesa nyingi, unajua sio juzi. Ni 1989 huko.”

Jambo lingine ambalo mtangazaji huyo wa Gidi na Ghost asubuhi alifichua ni alama zake za sekondari ambapo alisema alifaulu vizuri sana.

“Nilipata alama nzuri juu nilihitimu kwenda High school. Nilipata alama nzuri kusema kweli, sikumbuki ni nini lakini nilipata alama nzuri lakini nilihitimu nikaingia form 5 na form 6,” alisema.

Kuhusu vile angekuwa kama asingekuwa mtangazaji wa Redio, alisema, “Kama nisingekuwa Mtangazaji wa Redio, ningekuwa KDF ama ningekuwa KWS. Ningekuwa mtu nashughulika na wanyama.