Katumia mimba kama chambo

‘Nilimnasa kutumia uja uzito’

Wakati mwingi umesikia kuhusu mtindo wa wanawake kutumia mimba kuwanasa wanaume ili wawaoe.

Muhtasari
  • Edith alijua kweli njama yake imefaulu na sasa hapakuwa tena na hofu ya kuachwa na mume wake.
  • Alipojifungua, maisha yalionekana kuchukua safari aliyopanga

 

Simulizi za watu mbalimbali zitakupa  taswira ya hali zilizowapelekea kuolewa au kuoa mtu ambaye wako naye pamoja kwa sasa lakini baadhi ya hali zilizosababisha wanandoa kujipata pamoja zinatisha na  nyingine zinachekesha.

Wakati mwingi umesikia kuhusu mtindo wa wanawake kutumia mimba kuwanasa wanaume  ili wawaoe. Iwapo ulifikiri kwamba mtindo huo umepitwa na wakati au haufanyi kazi, basi Edith  atakushawishi kivingine kwa sababu hali yake iliyomfanya mchumba wake aliyetaka kumuacha kuamua kufunga pingu za maisha naye ni kama drama kutoka filamu ya naija. Baada ya uhusiano wa miaka miwili, Edith alianza kugundua kwamba mwenzake alikuwa ameanza kuboeka na kila jambo katika uhusiano wao halikuwa linampa uchangamfu. Wanavyosema wanawake wana uwezo mkubwa sana wa kujua hisia mbalimbali Edith alianza kugundua kwamba huenda uhusiano wao haungeishia katika ndoa kama alivyopanga na hapo ndipo alipoamua kutumia mtindo uliotumiwa na wengi mbele yake kuhakikisha kwamba anaolewa  na yule jamaa. Ni kipi kingine kingemfanya mwanamme kumvisha pete haraka isipokuwa mtoto?

Kupitia ushauri wa wanawake wenzake wanapopiga domo na daku daku kuhusu vitu  mbalimbali kuhusu wanaume, wengi walimshauri kwamba njia bora ya kumnasa mpenzi wake katika ndoa ni kupata mimba yake. Na baada ya kusitasita iwapo mpango huo ungefaulu, Edith aliamua kupiga moyo konde na kutumia mtindi huo na kwa kweli haikuwa rahisi lakini hatimaye aliweza kufaulu ingawaje gharama aliolipia kwa hatua hiyo imerudi kumpa kichapo. Alianza sasa kula njama kimya kimya kwamba angeshika mimba ya mpenzi wake  kisha aitumie kama chambo cha kumshawishi wafunge ndoa kama mume na mke. Alipopata ujauzito kama alivyotaka, basi alikuwa ameridhika akijiambia kwamba mpango wake upo katika mkondo wa kufaulu. Alipomueleza mwenzake kilichotokea, hakushtuka na akakubali kwamba sasa ilikuwa imetimu  hatua kwa wao kuanza maisha kama mke na mume isitoshe walikuwa wanamtaraji mtoto.

Alipojifungua, maisha yalionekana kuchukua safari aliyopanga. Mpenzi wake ambaye sasa alimtambulisha kama mume wake alitekeleza majukumu yake vyema na hata alifurahi sana kuitwa baba mtoto. Edith alijua kweli njama yake imefaulu na sasa hapakuwa tena na hofu ya kuachwa na mume wake. Ila hakuwa amepangia kitu kimoja. Siku hizi, usitumie mimba kama chombo cha kumnasa mwanamume kwa sababu pindi mtoto alipofika umri wa kuweza kuzungumza, dalili zile za kuachwa na mpenzi wake  ziliibuka.

Ugomvi kati yao sasa ulianza kuzagaa na kuwa wa kila mara huku  mwanamume akianza kusema jinsi anavyotaka kumpeleka mtoto wake kwa mamake nyumbani ili Edith aende zake. Haikuwa siri sasa kwamba mume wake alikuwa ameshagundua kwamba Edith alishika mimba ile maksudi ili kumnasa katika ndoa. Mpango huo ulionekana kutibuka wakati mume wake alipoonyesha mapenzi kwa mtoto na kuonekana kutojali kabisa kwa mama mtoto-Edith. Haikuchukua muda mrefu  kwa Edith kugundua kwamba ilikuwa hatari kwake kuendelea kuishi na mtu kwa lazima ilhali moyo wake na mipango yake haikuwa katika ndoa ile na papo hapo alikata kauli ya kujiondoa. Laiti angelitoka mapema bila ujauzito basi angesalia kuwa mwanamwali  mwenye uwezo wa kuolewa na mtu mwingine lakini  makovu ya uzazi na   kuzongwa na fikra chungu nzima kuhusu mwanamme asiyempenda yalimfanya Edith kuonekana kama mwanamke aliyekuwa ameolewa kwa mwongo mmoja .