Peter Kilonzo amekuwa akijaribu kwa miaka kadhaa kuileta pamoja familia yake baada ya mzozo kuhusu ugavi wa shamba kuigawanya na kuleta uhasama ambao umedumu kwa miaka kumi .
Tatizo lilianza wakati dada zake watatu walioolewa waliporejea nyumbani kwao baada ya kukosana na waume zao .waliihi kwa muda mrefu nyumbani bila kurejea katika maboma yao na mama yake akaamua kwamba basi wakati wa kugawana shamba ,nao wasichana pia wangepewa mgao wao . Hatua hiyo haikuwafurahisha kaka zake wawili ambao walinuna na kuhama kutoka nyumbani kwao . Kila mmoja alinunua ardhi yake na kuishi kivyake .
Kilonzo anasema kakake mkubwa na mdogo wake hawajazungumza na baba yao kwa takriban miaka kumi tangu mzozo ulipoibuka kuhusu ugavi wa shamba la familia . Kaka zake wanasema haitakuwa sawa shamba hilo kugawiwa dadake watatu ambao tayari walishaolewa na kurudi bomani ilhali hawajafanya matambiko ya kutalakiana rasmi na waume zao . Tofauti hiyo imeigawanya kabisa familia yao na mgawanyiko huo ulidhihirika wakati baba yao alipopata ajali na kuvunjika mguu .
Hakuna kati ya kaka zake waliotaka kumsaidia Mzee na kwa wiki mbili akiwa na jeraha alisalia nyumbani kwa uchungu . Majirani na jamaa zao walishangaa ilikuaje kwamba mzee ambaye alikuwa na watoto saba aliachwa kwa njia ile nusura afe kwa ajili ya jeraha lile kwa ajili ya uhasama uliotokana na ugavi wa shamba .
Mambo yamefanywa kuwa mabaya zaidi baada ya kugunduliwa kwamba mama yao ameegemea upande wa wasichana na kumshawishi Mzee kuwapa watoto wa kike hati za kumiliki shamba lao na kuzua zogo hata zaidi kati yao na kaka zao .
Kilozno amekuwa katikati ya mzozo wa familia yake kwa sababu sasa yeye ndiye aliyeachwa kama mpatanishi kwani kaka zake wanazungumza naye lakini hawazungumzi na wazazi wake. Wazazi nao sasa wakijipata mashakani wanapigia Kilonzo na katu hawawezi kuwasiliana na kaka zake wawili ambao waliamua kujitenga na familia yao.