Je ni akina nani wamefariki Tanzania mfululizo na kwa kipindi kifupi na kwa sababu zipi?

Muhtasari

•Vifo vya watu mashuhuri vimetikisa zaidi kwa sababu wengi wao maisha yao yanawagusa watu wengi.

Balozi Mahiga, mwanadiplomasia nguli aliyehudumu kwa miongo mitano, alifariki mwezi Mei, 2020
Balozi Mahiga, mwanadiplomasia nguli aliyehudumu kwa miongo mitano, alifariki mwezi Mei, 2020

Walatini wana msemo maarufu; Mors certa, incerta vita. Kwa tafsiri ya Kiswahili maneno hayo yana maana " kifo ni lazima, kuishi ni bahati". Msemo huu mara nyingi humaanisha kwamba katika maisha ya binadamu, jambo la uhakika zaidi kuliko yote mengine ni kwamba kuna siku mwanadamu ataondoka duniani.

Hata hivyo, wakati vifo vinapotokea kwa watu wengi - maarufu na wasio maarufu na tena katika kipindi kifupi na kwa mfululizo, hilo haliwezi kuwa jambo la kawaida. Na wakati vifo hivyo vinapotokea katika wakati dunia inakumbana na tatizo lililotangazwa na shirika la afya duniani (WHO kuwa ni janga; maswali yanakuwa mengi zaidi.

Ndiyo hali inayoikumba nchi ya Tanzania kwa sasa. Katika kipindi cha takribani mwaka mmoja kuanzia Machi mwaka jana hadi Februari mwaka huu, kumekuwa na taarifa nyingi za vifo vya watu mashuhuri na wasio mashuhuri. Hata hivyo, vifo vya watu mashuhuri vimetikisa zaidi kwa sababu wengi wao maisha yao yanawagusa watu wengi. Wengine, maisha yao yanagusa nchi kabisa.

Hili ndilo jambo lililosababisha baadhi ya magazeti yanayochapwa kwa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania kuandika taarifa zinazoeleza mshtuko uliopo baada ya vifo hivyo. Ni mshtuko kwa sababu kinachotokea sasa hakijawahi kuonekana katika historia ya nchi tangu ipate uhuru wake zaidi ya miaka 60 iliyopita.

 

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Idara ya Taifa ya Takwimu (NBS), zilizotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, zinaonyesha kwamba kwa wastani, Watanzania tisa kati ya kila 1000 hufariki dunia kila mwaka hapa nchini.

Kama tutachukulia kwamba Tanzania ina watu milioni 60 sasa, maana yake mwaka huu ilikadiriwa watu 540,000 watapoteza maisha kwa sababu mbalimbali. Hizi ni takwimu rasmi za serikali. Lakini, shirika la ujasusi la Marekani, linaeleza kwamba kiwango hicho cha vifo (crude death rate) kinafikia watu saba kwa kila watu 1,000. Kwa sababu hiyo, Tanzania wanakufa watu wachache kwa mwaka kulinganisha na marekani kwa sababu kwa wao, kiwango ni wastani wa watu nane kwa kila wananchi 1000.

Kuna uwiano usio sawa baina ya mkoa na mkoa au mijini na vijijini. Mkoa wa Njombe, kwa mfano, kiwango ni watu 13.5 kwa kila watu 1000. Kwa maana hiyo, kama njombe ingekuwa ni nchi yenye idadi sawa na ya Tanzania, watu 810,000 wangekuwa wanakufa kila mwaka katika taifa hilo.

Unaweza pia kusoma:

Kwa hiyo, ni vigumu kufahamu idadi kamili ya watu wanaofariki kwa mwaka. Huwezi kusema mwaka huu idadi ni kubwa au ndogo lakini kitakwimu, unaweza tu kufanya makisio kutokana na taarifa kama hizo za NBS na Sensa.

Hata hivyo, kwa msomaji wa magazeti na mitandao ya kijamii nchini Tanzania, anaweza kuamini kwamba kuna uwezekano kwamba mwaka huu mmoja utakuwa umeweka rekodi ya kuwa na vifo vingi kulinganisha na miaka mingi ya nyuma

Kwanini na ni akina nani?

Wakati wa vikao vya Bunge vya kujadili bajeti mwaka jana, wabunge watatu akiwamo aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Augustine Mahiga, walifariki dunia wakati wa mkutano huo wa Bunge. Wengine waliofariki kwenye mkutano huo Julai mwaka Jana walikuwa ni aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Gertrude Lwakatare na aliyekuwa Mbunge wa Sumve, Richard Mganga Ndasa.

Mchungaji Getrude Lwakatare ambaye pia aliyekuwa mbunge wa viti maalum nchini Tanzania, alifariki mwezi Mei, 2020
Mchungaji Getrude Lwakatare ambaye pia aliyekuwa mbunge wa viti maalum nchini Tanzania, alifariki mwezi Mei, 2020

Katika historia ya Bunge la Tanzania huru, haijawahi kutokea kwa wabunge watatu kupoteza maisha wakati wa mkutano mmoja wa Bunge. Wabunge hao walikuwa ni wa mkutano mmoja tu lakini mwaka huu pekee, tayari wabunge wengine wawili wamefariki dunia kwa sababu tofauti; Martha Umbulla kwa kuugua na Atashasta Nditiye kwa ajali ya gari.

Wabunge hao watatu wote walionekana kuwa na afya njema na walikuwa Dodoma kushiriki mkutano huo. Taarifa za vifo vyao zilishtusha watu wengi kwa sababu vyote vilikuwa vifo vya ghafla na vilivyofanana na vingine vya wananchi wengine.

Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin William Mkapa alifariki dunia mwezi Julai, 2020
Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin William Mkapa alifariki dunia mwezi Julai, 2020

Katika wakati akina Mahiga na Ndasa wanafariki dunia, kulikuwa pia na taarifa nyingine za Watanzania katika maeneo mbalimbali waliokuwa wakitajwa kufa kwa wingi na kulikuwa na video kadhaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha watu wakizikwa.

Pamoja na wabunge hao, mwaka jana na mwaka huu tumeshuhudia pia watu wengine mashuhuri kama rais mstaafu, Benjamin Mkapa, waziri mstaafu Arcardo Ntagazwa, Augustino Ramadhani, Nsa Kaisi, Bakari Mwapachu, Dk. Masumbuko Lamwai, Askofu Anthony Banzi, Asha Muhaji na Khalifa Ilunga (C Pwaa) aliyekuwa msanii mashuhuri wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini.

Wanahabari pia wamekumbwa na misiba katika wakati huu ambapo mwandishi mkongwe, Jimmy Mdoe na mwingine mwandishi mashuhuri wa habari za mazingira, Vedasto Msungu, nao walifariki dunia katika kipindi cha ndani ya wiki moja tu.

Kifo cha ghagla cha Mchungaji Maarufu wa Kanisa la Ghala la Chakula cha Uzima Peter Mitimingi, kilichotokea kiliwashitua wengi
Kifo cha ghagla cha Mchungaji Maarufu wa Kanisa la Ghala la Chakula cha Uzima Peter Mitimingi, kilichotokea kiliwashitua wengi

Kati ya wikiendi iliyopita na usiku wa kuamkia Februari 22 mwaka huu, Tanzania imepoteza wachumi wawili ambao ni miongoni mwa wachumi bora zaidi ambao taifa limewahi kuzalisha; Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile. Wawili hawa walihusika kwa kiasi kikubwa kwenye ujenzi wa sera za kiuchumi za nchi yao kwa kipindi cha muongo mmoja na nusu uliopita.

Tasnia ambazo zinaoneka kukumbwa na misiba kila uchao ni kama vile wanasheria, waandishi, viongozi wa dini na wanasiasa ambao kazi zao zinafanana kwa vile wanatakiwa kukutana na watu mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao.

Katikati ya Januari mwaka huu, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kilitoa orodha iliyoonyesha takribani dazeni ya majina ya wanasheria waliopoteza maisha tangu kuanza kwa mwaka huu pekee. Taarifa hiyo ilitolewa na rais wa tls, rugemeleza nshala na iliibua mjadala mrefu katika jamii ya watanzania mitandaoni na zaidi katika duru za mawakili na tasnia ya sheria kwa ujumla.

Nini chanzo cha vifo hivi?

Dunia nzima sasa inalia na ugonjwa wa Korona ambao umethibitishwa kuua mamilioni ya watu duniani na kuacha mamilioni wengi zaidi wakiwa bado wanaugua au wamewahi kupata maambukizi ya virusi hivi.

Maalim Seif Shariff Hamad alifariki dunia wiki iliyopita baada ya kuugua ugonjwa wa Korona
Maalim Seif Shariff Hamad alifariki dunia wiki iliyopita baada ya kuugua ugonjwa wa Korona

Kwa namna baadhi ya vyombo vya habari vinavyoripoti kuhusu vifo vinavyoendelea kutokea nchini Tanzania, ni rahisi kuhusisha ugonjwa wa Korona na vifo hivyo. Hata hivyo, ukweli ni kwamba si kila anayekufa ghafla au kwa magonjwa mengine wakati huu ni kwa sababu ya ugonjwa huo. Ni muhimu kurudi kwenye takwimu zinazotuambia kwamba hata pasipo Korona, watu zaidi ya 500,000 walikuwa wafe mwaka huu.

Lakini, si sahihi pia kusema kwamba miongoni mwa waliofariki dunia ni Maalim Seif Shariff Hamad pekee ndiye aliyefariki kwa ugonjwa huo kwa sababu tu chama chake cha ACT Wazalendo kilipata maono na ujasiri wa kutangaza ugonjwa wake.

Familia za marehemu wote waliotangulia mbele ya haki katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita zinajua nini vilikuwa vyanzo vya vifo hivyo. Watanzania wana tabia ya kutoa majina mengi yasiyo rasmi kama tafsida au namna ya kuepuka matatizo na mamlaka zinazotawala.

Kwa sababu msimamo wa serikali kuhusu ugonjwa wa Korona unajulikana, Watanzania sasa wanaita ugonjwa huo "changamoto ya upumuaji" ikiaminika hiyo ni njia salama kutoa taarifa kwa wahusika kuhusu sababu za kifo na wakati huohuo kukwepa kuingia kwenye matatizo na vyombo vya dola.

Kwa sababu Watanzania ni watu wanaosikiliza na kufuatisha maelekezo ya viongozi wao - tabia hii inaweza pia kufanya kazi nyingine; ya kuwaeleza nini hasa wanatakiwa kufanya ili kulinda uhai wao katika nyakati hizi ngumu.