SIASA ZA 2022

Kenyatta, Ruto na Odinga: Gharama halisi ya mapenzi ya siasa ya Kenya

Je ripoti ya BBI ndio suluhisho la amani na umoja wa kudumu Kenya

Muhtasari

•Ishara ya kwanza ya kuvunjika kwa ndoa hiyo ilijitokeza mwaka 2018, wakati rais alipomtangaza hasimu wake wa zamani, Bw Raila Odionga, kama mshirika wake wa tatu katika 'ndoa'.

•Nchini Kenya ndoa za kisiasa mara kwa mara huwa hazifungwi kwa msingi wa fikra - huwa zinawaleta pamoja watu maarufu kutoka makabila tofauti ambao maslahi yao huwa tu ni kupata mamlaka ya taifa na kuweza kufikia upatikanaji usio na ukomo wa utajiri wa taifa.

Image: GETTY IMAGES

Katika msururu wa barua zetu kutoka kwa waandishi wa habari wa Afrika, mkufunzi wa uandishi wa habari na mawasiliano Joseph Warungu anaangazia kuvunjika kwa ndoa ya kisiasa baina ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na naibu wake, pamoja na mtu wa tatu katika mahusiano yao tata.

Kenyatta alikuwa na umri wa miaka 51 wakati walipoingia mamlakani, huku Ruto akiwa na umri wa miaka 47.

Mwanasiasa waliyemshinda, Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, alikuwa na umri wa miaka 68 wakati huo.

Alinadiwa kama mkongwe na mzee wa kizazi kilichopitwa na wakati ambacho ni cha nyakati mbaya na kilichosahaulika, huku wanandoa ''vijana'' walinadiwa kwa maneno ya kisasa - wanandoa wa digitali.

Miaka minane na chaguzi mbili baadaye, ndoa ilivunjika na sisi, watoto wao, raia wa kawaida wa Kenya, wamepotea.

'Handshake'' iliyobadili siasa

Ishara ya kwanza ya kuvunjika kwa ndoa hiyo ilijitokeza mwaka 2018, wakati rais alipomtangaza hasimu wake wa zamani, Bw Raila Odionga, kama mshirika wake wa tatu katika 'ndoa'.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2017, Bw Odinga ambaye alikuwa katika ndoa nyengine ya kisiasa katika Muungano wa Nasa, na washirika wengine watatu, alikua ameanzisha wimbi la maandamano akidai kwamba uchaguzi haukuwa wa haki na huru.

Kutokana na hofu kwamba maandamano hayo yangekwamisha juhudi zake za kutekeleza ahadi zake katika muhula wa mwisho mamlakani, Rais Kenyatta aliwasiliana na Bw Odinga na wawili hao wakasalimiana kwa mikono mbele ya umma kama azimio la amani.

Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga
Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga
Image: Hisani

Taratibu, Bw Ruto akaanza kujiondoa kutoka kwa mwenzi wake wa miaka mitano, akilalamika kuwa ndoa ilikuwa imejaa umati wa watu.

Leo, ugumu wa mahusiano baina ya wenza hao wawili unaoneshwa wazi hadharani.

Ruto alikataa kutoka kwenye ndoa, Bw Odinga amehamia katika nyumba ya wanandoa, na kama wanavyofanya wake wapya, anaonekana kupendwa zaidi na kumvutia Bw Kenyatta ambaye kamwe hana aibu ya kumsifu hadharani.

Wakati wa sherehe za Uhuru wa Kenya tarehe 1 Juni, Rais alitangaza kuwa amepata mafanikio makubwa ya kimaendeleo zaidi katika muda aliokuwa nao na Bw Odinga kuliko wakati alipokuwa na Ruto.

Hatahivyo, Bw Ruto mwenye hasira amekataa kujiuzulu-au kuondoka katika nyumba ya wanandoa. Hutumia muda wake katika chumba cha wageni, akilalamika kwa kila yeyote anayejali kumsikiliza kuwa alitelekezwa licha ya kumsaidia bosi wake kujenga himaya.

Wakati wawili hao walipoungana, walikuwa na makubaliano 20 ambayo hayakuandikwa kwenye karatasi, ambapo Bw Ruto angemuunga mkono Kenyatta kuhudumu kama rais kwa mihula miwili ya miaka mitano mitano.

Baada ya hapo Bw Kenyatta ''angerudisha mkono'' kwa kumuunga mkono naibu wake katika uchaguzi wa 2022 na yeye pia ahudumu kwa mihula miwili, miaka 10 kwa ujumla.

Lakini Januari 2021 rais alitoa azimio la wazi kwamba mkataba huo ulikufa.

"Urais sio wa makabila mawili tu," rais aliuambia umma uliokusanyika, akiongeza kuwa labda wakati umefika kwa makabila mengine 42 ya Kenya kuchukua uongozi wa nchi.

Rais Kenyatta alisema kuwa ni makabila mawili pekee ambayo yameongoza kiti cha urais nchini Kenya- Wakikuyu na Wakalenjin.

Je ripoti ya BBI ndio suluhisho la amani na umoja wa kudumu Kenya

Bw Kenyatta ni Mkikuyu na Bw Ruto ni Mkalenjini huku Bw Odinga akitoka katika kabila la Wajaluo, ambalo limekuwa likilalamika kwa muda mrefu kwamba limekuwa likitengwa na mamlaka.

Nchini Kenya ndoa za kisiasa mara kwa mara huwa hazifungwi kwa msingi wa fikra - huwa zinawaleta pamoja watu maarufu kutoka makabila tofauti ambao maslahi yao huwa tu ni kupata mamlaka ya taifa na kuweza kufikia upatikanaji usio na ukomo wa utajiri wa taifa.

Kenya imegawanyika

Bw Ruto hakubaliani na hoja kwamba Wakalenjin hawawezi kutawala tena au kwamba hawezi kuungana, kwa mara nyingine tena, na Wakikuyu watoro.

Kwa sasa amechukua njia ya vita vya kisiasa, na kufanya ziara za mara kwa mara kati kati mwa Kenya kuwarai Wakikuyu.

Anapigania ndoa yake na anataka ulinzi wa watoto wake.

Na sisi, watoto tumekwama kwa kuwa na mapenzi kwao wote wawili.

Je tubaki na baba ambaye anapaswa kustaafu urais mwaka ujao?

Image: AFP

Tunajiuliza je tumpokee mwenza wake mpya Bw Odinga, ambaye anatupatia hali ya amani ya siku zijazo na jamii yenye usawa zaidi, yenye mchanganyiko wa muziki wa rege ambao huwa anauimba mara kwa mara anapokuwa jukwani wakati anapokampeinia mabadiliko ya katiba?

Au tumfuate Bw Ruto - mpenzi wa zamani, ambaye ni jasiri, mkakamavu na anayeahidi matumaini kwa wengi ambao wanahangaika kutafuta riziki yamaisha?

Kuvunjika kwa ndoa ya urais nchini Kenya kumekuja kwa garama kubwa. Kuvunjika kwa nyumba ya wanandoa.

Watoto wanaumia

Taasisi za kifedha za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Benki ya dunia na Shirika la fedha duniani (IMF) , ilibidi ziingilie kati kwa madeni kusaidia kuziba pengo la upungufu wa bajeti ya taifa.

Malipo yataumiza. Mashirika haya yanadai kufanyika kwa mabadiliko ya taasisi zinazodhaminiwa kwa garama kubwa na umma, ikiwa ni pamoja na baadhi ya vyuo vikuu na Shirika la safari za ndege la Kenya-Kenya Airways. Hii itamaanisha kupunguzwa kwa wafanyakazi.

Image: GETTY IMAGES

Bei za bidhaa muhimu kama vile mafuta, data za simu za mkononi na gesi ya kupikia zimepanda juu.

Talaka huwa haiwi nafuu . Inaumiza, inaleta msongo wa mawazo na kuchosha kihisia.

Huku wazazi wanaoachana tayari wanawatazama wapenzi wengine wa kisiasa, watoto hawananyumba nyingine ya kuishi isipokuwa Kenya.

Kuna ishara kwamba uchaguzi mkuu uliopangwa mwaka ujao unaweza kuahirishwa ili kuwezesha kufanyika kwa marekebisho ya katiba, ikiwa ni pamoja na ukuongeza ukubwa wa baraza la mawaziori na kubuni majimbo zaidi ya bunge.

Watoto masikini wana hofu kwamba maumivu yao yanaweza hata kuongezeka zaidi