Hofu ya wakazi wa Merti , Isiolo

NRT ni shirika la kuhifadhi wanyamapori ambalo limekuwa likiendesha shughuli zake Kaskazini mwa Kenya tangu mwaka 2004

Muhtasari

• Mama Khadija ambaye ni mjane hana uhakika iwapo ardhi ya jamii ambayo amekuwa akiitumia kuwalisha mifugo kwa kipindi cha miaka 54 itakuwepo miaka michache ijayo.

• NRT inasema kuna dhana potofu dhidi ya shirika hilo, yataja umuhimu wa jamii kuhamasishwa kuhusu mipango yake.

Baadhi ya ngamia wa wafugaji wa jamii ya Waborana
Baadhi ya ngamia wa wafugaji wa jamii ya Waborana
Image: Shisia Wasilwa

Jua linapochomoza katika kaunti ya Isiolo, viungani mwake katika eneo la Merti, mama Khadija ameketi nje ya nyumba yake ya usonge.

Nguvu zake na ari ya maisha vinamsaliti kutokana na kalenda nyingi alizokula. Anakonyeza macho yake mbinguni kana kwamba anatafuta majibu ya maswali yanayomtekenya ubongo. Mama Khadija ambaye ni mjane hana uhakika iwapo ardhi ya jamii ambayo amekuwa akiitumia kuwalisha mifugo wake kwa kipindi cha miaka 54 itakuwepo miaka michache ijayo.

“Vitendo vya NRT ni vibaya. Mimi hakuna mtu ambaye ameniuliza kuhusu hifadhi ya wanyamapori,” Khadija anateta huku akinikazia macho.

Tayari kipande kikubwa cha ardhi cha majirani zake katika kaunti ya Samburu, kimeshatwaliwa na shirika binafsi la kuhifadhi wanyamapori la Northern Rangers Trust (NRT) na sasa kipande cha ardhi cha malisho katika eneo lake kinalengwa.

“Wasamburu wanalazimika kuleta mifugo wao kwa malisho hapa Isiolo, kwa maana hawana ardhi ya malisho. Yote imechukuliwa.” Khadija anaoongeza.

NRT ni shirika la kuhifadhi wanyamapori ambalo limekuwa likiendesha shughuli zake Kaskazini mwa Kenya tangu mwaka 2004. Kwa sasa lina hifadhi 39 Kaskazini mwa Pwani ya Kenya. Ekari 42000 ambazo ni sawa na asilimia nane ya ardhi yote ya taifa imo mikononi mwao. Mbali na mji wa Isiolo wenye majengo ya kupendeza, biashara inayonoga na uwanja wa kisasa wa kimataifa wa ndege, safari ya saa tano kwenye barabara ya vumbi jingi na joto la kuunguza, lanifikisha katika eneo la Merti.

Merti ni eneo tambarare lisilo na wakazi wengi, miundo msingi bora lakini lenye watu wakarimu na tabasamu usoni. Barabarani nawaona swara, nyani na wanyamapori wengine. Saa sita kamili, jua limeshitadi, nyuzi joto 37. Mavazi yangu yameroa na kusakama vumbi. Nywele zangu nyeusi zimebadilika rangi na kuwa hudhurungi kwa kushiba vumbi. Nafika mahali mkutano wa kulitafutia ufumbuzi suala la NRT linapofanyikia.

Wazee wameketi mduara chini ya mti wa mkambaa unaotapakaza kivuli cha kutosha. Wamekuwa wakikutana kila mara kujadili vitendo vya NRT vinavyotisha kubadilisha mkondo wa maisha yao. Kwa saa kadhaa, nawasikiza. Kila mmoja akitapika hasira na ghadhabu dhidi ya shirika hilo. Mkutano wa leo umehudhuriwa na waatalamu mbali mbali katika jamii hii, wakiwemo walimu, mawakili na watetezi wa haki za binadamu wanaotoa hamasisho.

Mifugo wa wafugaji
Mifugo wa wafugaji

Ismael Huka ana umri wa miaka 60. Anapangusa kijasho kinachotiririka usoni na kuishia kwenye masharubu yake aliyopaka rangi ya zambarao. Msimamo wake ni dhabiti dhidi ya NRT.

“Ardhi hii ni raslimali yetu. Tunahitaji hati miliki sasa. Mababu zetu wamekuwa wakiishi na wanyamapori kwa miaka mingi na wamekuwa wakiwahifadhi.”

NRT tayari wana hifadhi moja ya wanyamapori Katika eneo hili la Merti la Biliqo-Bulesa ambalo lilianzishwa mwaka 2006. Wazee hawa wanaimani na matarajio kama tu jimbo la Turkana lilivyolitimua shirika la NRT, ndivyo nao pia wanavyopanga kufuata nyayo zao.

Osman Abedi, ni mzee mwenye umri wa miaka 63. Ndiye mwenyekiti wa baraza la wazee. Anadai kuwa tangu NRT waanze shughuli zao, kumekuwepo na ongezeko la bunduki haramu. NRT lina kikundi chake cha maafisa wa usalama walio na bunduki. Ni mmoja kati ya waliohudhuria semina iliyoandaliwa na NRT, kujadili suala la kuanzisha hifadhi. Anadai kuwa shirika hilo halikutoa ripoti kuhusu ubaya na uzuri wa kuwa na hifadhi ya wanyamapori katika eneo hili kama walivyoafikiana na wakazi.

“Hii ni ardhi ya jamii. Haijasajiliwa. Zaidi ya watu 50 wameuawa tangu mwaka huu uanze, kutokana na bundiki zinazopatikana kwa urahisi,” Osman ananifahamisha.

Hifadhi za Wanyamapori za Jamii zinaendelea kuongezeka nchini Kenya, huku zikifadhiliwa na mashirika ya kimataifa, mashariki ya serikali na yasiyo ya serikali.

Mtaalamu wa masuala ya usalama katika upembe wa Afrika Abdullahi Boru anasema kuwa, hilo limechangiwa na vipande vikubwa vya ardhi vinavyopatikana katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya ambayo hayakaliwi na watu wengi. Boru anasema kuwa hifadhi hizi zinapatikana mbali sana ambapo inakuwa vigumu kwa serikali kufikia na kutoa huduma za msingi. Hivyo NRT inachukua fursa hiyo na kujaribu kujaza mapengo au majukumu ya serikali kama vile usalama, kuzuia wizi wa mifugo na hata kujenga vituo vya afya.

Hata hivyo kumekuwa na malalamishi mengi kutoka kwa wakazi likiwemo ukiukwaji wa haki za binadamu. Halkano Abdullahi ni wakili. Kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita amekuwa akiihamasisha jamii hii kuhusu haki zao.

“Tunawafunza haki zao kuhusu ardhi yao. Kwa sasa tumemaliza uhamasisho. Tunaanza mchakato wa kusajili ardhi yao sasa,” Halkano anafafanua.

Adan Diba ni mwenyekiti wa Amani na Usalama katika jimbo hili ndogo la Merti. Ni miongoni mwa wazee wanaohudhuria mkutano wa kutafuta mwarubani kwa vitendo vya NRT. Anasema kuwa hifadhi za wanyamapori za jamii huathiri sio tu usalama wao, lakini pia haki zao, utamaduni na turathi zao.

Ninapomuuliza Diba kile watakachokifanya, iwapo kilio chao na juhudi zao havitazaa matunda, uso wake unamwanguka, anayatorosha macho yake kwa unyonge kisha kwa sauti ya kumsaliti anasema: “Sisi ni raia tu. Kuna mahali ambapo juhudi zetu haziwezi kufika.”

Huku wazee wakiafikiana kusitisha shughuli za NRT kwa umoja na utele, mama Halima Kampicha mwenye umri wa miaka 50, amesimama kidete dhidi ya wazee hawa. Anaupinga msimamo wao kwa kinywa kipana. Kwake wanaopinga miradi ya NRT wanatumika na wanasiasa kudemaza mipango itakayonufaisha jamii nzima.

“Hawa wazee, wengi wao wanatumika tu na wanasiasa. Hawana ufahamu wowote kuhusu yanayojiri,” Halima ananifahamisha kwa hasira.

Wazee katika eneo la Merti wakutana kujadili mipango ya shirika la NRT
Wazee katika eneo la Merti wakutana kujadili mipango ya shirika la NRT
Image: SHISIA WASILWA

Mpango wa Hifadhi za wanyamapori za jamii ulijumuishwa kwenye sheria mwaka 2013. Waasisi wake walishikilia kuwa asilimia 70 ya wanyamapori nchini Kenya wanapatikana nje ya hifadhi za taifa, na uhai wao unategemea uhifadhi wa ardhi kubwa zinazomilikiwa na jamii na watu binafsi. Ukosefu wa uwazi na ufahamu wa kutosha kwa jamii ni baadhi ya mambo yanayowapa wasiwasi wakazi hawa kuhusu unyakuzi wa ardhi zao.

Mbunge wa Isiolo Kaskazini Hassan Odha na Mwakilishi wa wanawake wa jimbo hilo Rehema Jaldesa, wameapa kusitisha shughuli zote za NRT kutwaa kipande chochote cha ardhi yao.

“Mswada wa hifadhi ya wanyamapori wa Isiolo, haujazingatia wakazi wa Isiolo. Una manufaa zaidi kwa NRT. Nilikuwa mmoja wa watu walioujadili lakini ulipochapishwa, mswada wenyewe umebadilishwa. Ni tofauti na yale ambayo tulijadili kabla uchapishwe,” Hassan anasema.

Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu nchini Kenya, ilitoa taarifa ya tahadhari kwa bunge la jimbo la Isiolo kuhusu mswada wa kuhifadhi wanyamapori katika jamii. Tume hiyo inapendekeza kuwa bunge hilo lisitishe mijadala yoyote kuhusu mswada huo hadi ardhi yote ya jamii isajiliwe. Mswada huo uliowasilishwa mapema mwaka huu, umedhaminiwa na NRT. Mswada huo unapendekeza kubuniwa kwa sheria ya kuhifadhi wanyamapori katika jimbo la Isiolo, kuanzishwa kwa halmashauri za kuhifadhi wanyamapori za jamii na mfuko wa kuhifadhi wanyamapori.

Akizungumza kupitia mahojiano ya simu, afisa mkuu mtendaji wa NRT Tom Lalaampa alipuuza madai yaliyotolewa dhidi ya shirika hilo.

“Kuna dhana potofu dhidi ya NRT, kuna haja kwa jamii kuhamasishwa. Watu wengi hawaelewi. NRT haina mamlaka juu ya ardhi. Ni jamii ambayo inatumika kujiunga na NRT kwa uhifadhi. Tunapokea maombi mengi kutoka kwa jamii ambazo zinataka kujiunga na NRT na sio njia nyingine.

Kituo cha Merti
Kituo cha Merti

Lalampaa ambaye amekuwa msimamizi wa shirika hilo kwa miaka miwili iliyopita alisema kwamba hawajawahi kunyakua ardhi yoyote.

"Tunapopokea maombi kutoka kwa jamii ambayo inataka kujiunga nasi, tuna bodi ambayo inatoa utaratibu wa kujiunga na kuwasilisha ombi hilo kwa serikali ya kaunti kwa mchakato kuanza." Ananiambia huku akicheka.

Lalampaa anasema jamii zingine huko Samburu zimeelewa na kukubali kufanya kazi na NRT.

"Hifadhi za jamii zinaendeshwa na jamii, anaongeza. Jukumu letu ni kuwasaidia katika kuhifadhi rasilimali. "

Tangu mapema mwaka wa 2000, kumekuwepo na ongezeko la hifadhi za wanyama pori katika kaunti za wafugaji za Baringo, Samburu, Turkana, Pokot Magharibi, Laikipia, Isiolo, Marsabit na Garissa. Mara nyingi jamii hizo zimejipata zikikwaruzana na mashirika yanayosimamia mipango hiyo. Katika jimbo dogo la Merti, lililoko katika kaunti ya Isiolo, baadhi ya wenyeji wanahofu kuwa maeneo yao ya malisho ya mifugo huenda yakatwaliwa na Shirika la Northern Rangers Trust (NRT) bila ya kuhusishwa kwenye mchakato mzima, mbali na kuwa hawana hati miliki za ardhi.

Mkutano wa wazee hawa, unafumukana, baada ya kujadili. Wanakubaliana kwa jambo moja kuwa, lazima wasajili ardhi zao, ndipo wafanye kikao na NRT, lakini kwa sasa hawatakubali. Jua linapoelekea magharibi mama Khadija aliyevalia hijabu anasema kuwa hatakubali NRT ipate hata kipande kidogo cha ardhi ambacho babu zake wamekuwa wakikitumia kwa malisho, pengine juu ya maiti yake.

Shisia Wasilwa ni Mwanahabari na pia mshauri wa masuala ya mawasiliano.

(Mhariri: Davis Ojiambo)