NASA hainasi tena ni ndoto, asema Mudavadi

Muhtasari

• Kinara huyu wa ANC alisema kuwa ahadi walizoafikiana kwenye mkataba wa NASA zimesalia kuwa tu kwa karatasi.

• Mudavadi alieleza kwamba falsafa yake ya kukomboa wakenya kutoka kwenye minyororo ya ufukara na ukosefu wa ajira itasalia kuwa mojawepo ya ajenda zake kuu.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi. Picha:HISANI
Kinara wa ANC Musalia Mudavadi. Picha:HISANI

Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi amesema kuwa kufufuliwa kwa muungano wa NASA ni kama ndoto na amefichua kuwa umaarufu wa Nasa umedidimia sana.

Akuzungumza siku ya Alhamisi Mudavadi alisema kuna masuala kadhaa ambayo yalifaa Kuafikiwa kwa mujibu wa mkataba wa NASA lakini mengi yamekwama.

Kinara huyu wa ANC alisema kuwa ahadi walizoafikiana kwenye mkataba wa NASA zimesalia kuwa tu kwa karatasi lakini utekelezwaji wake umezingirwa na misukumo ya kutoaminiana katika muungano huo.Mudavadi alikariri msimao wake kwamba yeye sio kibaraka na wala hana nia ya kuuza sera zake kwa misingi ya kiongozi mwingine.

Mudavadi alieleza kwamba falsafa yake ya kukomboa wakenya kutoka kwenye minyororo ya ufukara na ukosefu wa ajira itasalia kuwa mojawepo ya ajenda zake kuu kwenye safari ya kusaka urais wa taifa hili.

Mudavadi aliwataka wale ambao wanadai kuwa yeye ni kibaraka kujitokeza wazi na kutoa Ushahidi ambao utathibitisha hilo.

Alikashifu dhana hiyo na kusema kuwa wakenya wanafahamu fika kuwa uhusiaano wake na Rais Uhuru Kenyatta unaegemea pakubwa masuala yanayowahusu wakenya bali sio kufuta ushabiki wa kisiasa.

Aliwataka wakenya kujiuliza hasa ni mwanasiasa yupi ambaye yuko karibu na rais pakubwa na kujiondolea lawama kuwa yeye ni kiongozi mwenye msimamo huru huku akisema kuwa juhudi za kuimarisha chama cha ANC na kukwamua uchumi wa Kenya ndio malengo yake makuu.