'Aliniambia nipokua wake, sitakua wa mtu mwingine' Mwanamke asimulia alivyochomwa usoni kwa tindikali na mpenzi wake wa zamani alipokataa kumrudia

Muhtasari

•Mpenzi wake wa zamani na baba ya watoto wake wawili anayetuhumiwa kufanya shambulio hilo anazuiliwa kwa jaribio la mauaji.

Esmeralda Millán alishambuliwa kwa tindikali mjini Puebla, Mexico
Esmeralda Millán alishambuliwa kwa tindikali mjini Puebla, Mexico
Image: ANA GABRIELA ROJAS

Esmeralda Millán alikuwa na miaka 23 Disemba mwaka 2018 aliposhambuliwa kwa tindikali mjini Puebla, Mexico. Mpenzi wake wa zamani na baba ya watoto wake wawili anayetuhumiwa kufanya shambulio hilo anazuiliwa kwa jaribio la mauaji.

Hakuna maelezo rasmi kuhusu ni wanawake wangapi wamepitia unyanyasaji wa aina hii nchini Mexico. Lakini kundi linalowasaidia waathiriwa linasema limenakili visa 26, na sita kati ya visa hivyo vilifanyika mwaka huu.

"Sawa na unyanyasaji mwingine wowote dhidi ya wanawake, mashambulio haya yaliongezeka wakati wa amri ya kutotoka nje iliyowekwa na nchini tofauti kudhibiti maambukizi ya corona," anasema Norma Celia Bautista Romero, Mkurugenzi wa shirika la Humanismo y Legidad, ambalo linapigania usawa wa kijinsia.

"Aina hii ya unyanyasaji hufanywa kwa lengo moja tu. Wanaofanya hivi wanataka kumdhuru mwanamke na kila kitu anachosimamia.

Lengo ni kuhakikisha anasalia na alama ya maisha. Kusababisha mateso ya kudumu kimwili na kisaikolojia," anaeleza.

Asilimia 90 mashambulio ya aina hii hutekelezwa na wanaume na huwa wana uhusiano na wanawake wanaowashambulia.

Wanawake hao mara nyingi huwa ni wapenzi wa zamani. Katika baadhi ya matukio, mtu mwingine anatumwa kutekeleza shambulio.

Picha ya muonekano wa Esmeralda an kabla na baada ya kushambuliwa
Picha ya muonekano wa Esmeralda an kabla na baada ya kushambuliwa
Image: CORTESÍA ESMERALDA MILLÁN

Sikuwa nimetimiza miaka 15 nilipokutana naye na nilipofikisha umri wa miaka 17 nilijifungua mtoto wangu wa kwanza. Alianza kuninyanyasa nilipokuwa mjamzito.

Alininyanyasa kwa kila njia: alinipiga, kunilazimisha kufanya ngono na kunifanya nihisi nimenaswa nisijue la kufanya.

Nilipopata nafasi nilitoroka na kwenda kuishi na mama yangu, lakini alikuja kunichukua. Aliniambia kuwa hatarudia tena makosa hayo na kwamba atabadilika. Aliniambia yeye mwenyewe ni muathiriwa wa unyanyasaji kutoka kwa baba yake na kwamba hangelipenda kadhia hiyo ijirudie.

Alifanikiwa kunishawishi kurudi kwa nyumba yake. Lakini haikuchukua muda alianza tena kuninyanyasa. Nilipata ujauzito kinguvu mara ya pili na kujifungua mtoto wetu wa kike.

Hali ilipokuwa ngumu niliingiwa na mawazo ya kutengana naye, lakini nilihisi siwezi kufanya hivyo. Alinifanya nijihisi kwamba niko peke yangu na hakuna mtu atanisaidia isipokuwa yeye tu ambaye namtegemea.

Esmeralda Millán akiwa na shangazi, mama na bibi yake (kushoto kwenda kulia).
Esmeralda Millán akiwa na shangazi, mama na bibi yake (kushoto kwenda kulia).
Image: ANA GABRIELA ROJAS

Kwa hivyo nilivumilia mateso kwa miaka kadhaa. Hadi siku moja aliponipiga vibaya nikaamua kujitetea. Mwana wangu wa kiume ambaye wakati huo alikuwa na miaka saba aliingilia vita hivyo. Alitaka kunisaidia, Nikamuomba asimpige baba yake tena.

Wakati huo niligundua kwamba hayo sio mazingira mazuri ya kuwalea watoto wangu. Sikutaka waishi Maisha hayo ya vurugu. Niliwachukua na kurudi nao tena kwa mama yangu.

Nilimwambia tutawasiliana kwa ajili ya watoto na tukafikia uamuzi huo. Lakini aliendelea kusisitiza nirudi nyumbani.

Wakati mmoja alijaribu kunichukua kwa nguvu. Aliniburuza chini hadi kwenye pikipiki inayotumiwa kama teksi iliyokuwa karibu.

Kwa bahati nzuri watu waliokuwa karibu walinisaidia. Walihakikisha naishi mahali kuna watu wengi ili akijaribu kunishambulia tena wamchukulie hatua kwa idhini ya mjomba wangu aliyekuwa anaishi karibu na hapo.

Tangu wakati huo niliishi kwa uwoga, Sikutaka kuwa karibu naye tena. Niliomba familia yangu isimruhusu kufika mahali nilipokuwa naishi. Lakini aliendelea kunirai turudiane: lakini nilikataa kabisa.

Siku moja nilienda kuchukulia ada ya matumizi ya watoto. Mara akaniuliza kama siku iliyofuata nitakuwa na shughuli yoyote. Nikamwambia kwamba nimealikwa sherehe na marafiki zangu.

Kabla ya kuondoka aliniuliza tena nitatoka nyumbani saa ngapi siku iliyofuata kisha akaomba kunipiga pambaja. Nilikataa. Lakini alisisitiza sana. Aliahidi nikifanya hivyo hatawahi kunisumbua tena.

Nilipata usumbufu wa mawazo hadi niliporudi nyumba nikamwambia mama yangu kile kilichotokea.

Alinimwagia tindikali usoni

Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili, Disemba tarehe 2, 2018,alitoka kujivinjari na marafiki zake mwedo wa saa kumi na moja na nusu alfajiri. Bado kulikuwa na giza lakini aliona wanaume watatu wamesimama mbele ya nyumba yake.

Mara wakaanza kutembea kuja upande wangu na mwingine akarudi nyuma yangu. Nikitahamaki wamenizingira.

Tulipokaribiana ana kwa ana mmoja wao alinimwagia kitu kama maji usoni. Alipobaini kuna mengine yamebakia kwenye chupa, alinishika kichwa na kujaribu kunimwagia. Katika lile purukushani yeye pia alijimwagia maji hayo usoni.

Yeye pia alichomeka. Lakini lengo lake lilikuwa kuniona nikihangaika vibaya hivyo.

Na kutoka hapo nikagudua mshambuliaji alikuwa mpenzi wanngu wa zamani na baba ya watoto wangu wawili.

Esmeralda Millán akiwa na mama yake kabla ya kushambuliwa
Esmeralda Millán akiwa na mama yake kabla ya kushambuliwa
Image: ESMERALDA MILLÁN

Nilijua hilo kutokana na mwendo wake, pia kwa sababu nilikuwa mrefu kumliko. Alikuwa amevalia nguo sawa na ile aliyokuwa nayo nilipompelekea watoto. Alikuwa amejifunika uso asubuhi hiyo iliyokuwa na baridi kikali.

Niliishi naye kwa miaka tisa , naweza kumtambua vizuri sana bila shaka.

Na pia nilimtambua kwa sabau alisema mara kwa mara kwamba: " Ikiwa hutakuwa wangu, hutakuwa na mtu mwingine. "

Sikujua shambulio la tindikali ni nini. Sikujua kilichokuwa kinafanyika. Nilihisi kana kwamba ninakauka.

Nilikuwa nimemeza maji hayo na koo yangu ilikuwa inafungika. Sikuweza kupumua. Nilimsikia mama yangu akipiga mayowe, Sijawahi kumsikia akipiga mayowe namna hiyo tena.

Hakuna mtu aliyetusaidia. Hadi mama alipomuita shangazi yangu, ambaye alikuja kutupeleka. Nilihisi uchungu hadi nikapoteza fahamu.

Tindikali aliyonimwagia iliathiri vibaya uso wangu pua na mdomo. Iliniharibu jicho la kulia na mpaka sasa siwezi kuona upande mmoja.,

Esmeralda Millán amefanyiwa upasuaji zaidi ya mara 16 katika miaka ya hivi karibuni.
Esmeralda Millán amefanyiwa upasuaji zaidi ya mara 16 katika miaka ya hivi karibuni.
Image: ANA GABRIELA ROJAS

Tindikali pia ilinichoma shingo na mikono. Iliathiri koo vibaya sana hadi sikuweza kula kwa miezi miwili. Nililazwa hospitali kwa miezi mitatu.

Nilipoona uso wangu kwenye kioo nilihisi maisha yangu yamekwisha.

Nilipata msongo mbaya sana wa mawazo. Kwa muda mrefu nilitamani kufa.

Shambulio hilo halikuniumiza mimi peke yangu. Mama yangu na watoto wangu pia wameathirika sana. Imekuwa vigumu sana kwao kukubali muonekano wangu mpya. Mwanangu ameonewa shuleni.

Mwezi Disemba mwaka huu itakuwa miaka mitatu tangu aliposhambuliwa na mpaka sasa sitaki kuonesha uso wangu.

Kwanza watu walikuwa wakinilaumu, walisema nastahili kilichonikuta. Nililipia tu ada ya kutaka kumuacha mnyanyasaji.

Upasuaji mara 16

Nimefanyiwa upasuaji mara16. Uso wangu kidogo umekuwa nafuu, lakini sitawahi kurudi vile nilivyokuwa. Makovu ya majeraha aliyoniachai moyoni hayatawahi kupona.

Baba ya watoto wangu anawezaje kunifanyia hivi? Mtu anawezaje kuwa na chuki na kufanya ukatili wa aina hii?

Esmeralda Millán na Isela Mendez, daktari wa upasuaji ambaye alimsaidia
Esmeralda Millán na Isela Mendez, daktari wa upasuaji ambaye alimsaidia
Image: CORTESÍA ESMERALDA MILLÁN

Mshambuliji wangu, Fidel N, huenda akafungwa hadi miaka 40. Natumai hukumu itatekelezwa, naomba asitoke hivi karibuni. Nahofia hilo likifanyika, atakuja kunimaliza.

Kando na hilo, pia nataka washirika wake watatu pia wakamatwe.

Mchakato huo umekuwa ukifanyika kwa mwendo wa kinyonga kwa sababu amebadilisha mawakili mara tatu na pia vikao vya mahakama vimeahirishwa mara kadhaa kutokana na janga la corona.