Pandora Papers: Shakira, Guardiola, Di María wahusishwa na mali iliyofichwa katika akaunti za siri

Muhtasari

•Kuvuja kwa nyaraka za kifedha karibu milioni 12 zinazoonesha utajiri uliofichwa, kukwepa kodi na, wakati mwingine, utakatishaji fedha , sio tu kwa wafanyabiashara, wanasiasa na viongozi wa ulimwengu, lakini pia watu mashuhuri.

Image: BBC WORLD

Kuvuja kwa nyaraka za kifedha karibu milioni 12 zinazoonesha utajiri uliofichwa, kukwepa kodi na, wakati mwingine, utakatishaji fedha , sio tu kwa wafanyabiashara, wanasiasa na viongozi wa ulimwengu, lakini pia watu mashuhuri.

Waimbaji kama vile wa Uhispania Julio Iglesias na Shakira wa Colombia, nyota wa soka kama vile Muajentina Ángel di María na Pep Guardiola wa Uhispania ni miongoni mwa watu waliobainika kuwa na makampuni yaliyosajiliwa mataifa ya nje.

Kulingana na uchunguzi, wote ni wamiliki wa kampuni zilizo kwenye mataifa yenye nafuu ya kodi, ambayo ni halali ikiwa mmiliki ataweka wazi ni wapi makampuni hayo yalipo, lakini pia maeneo hayo hutumiwa mara nyingi "kuficha pesa taslimu au kuepuka ushuru ", kulingana na watafiti.

Zaidi ya waandishi wa habari 600 katika nchi 117 wamekuwa wakitafiti kwa vyanzo 14 kwa miezi, wakipata taarifa ambazo zinachapishwa wiki hii.

Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari wa Upelelezi (ICIJ) huko Washington DC, ilizipata data hizo, ambayo imekuwa ikifanya kazi na mashirika zaidi ya 140 ya habari kwenye uchunguzi wake mkubwa zaidi ulimwenguni.

Hawa ni baadhi tu ya watu mashuhuri ambao majina yao yamejitokeza kwenye uchunguzi.

Pep Guardiola

Image: MICHAEL REGAN / GETTY IMAGES

Gwiji huyo wa zamani wa Barcelona na meneja wa sasa wa Manchester City ni nyota mwingine wa soka kwenye nyaraka za Pandora

Hati hizo zinafichua kwamba Guardiola alikuwa mmiliki wa akaunti katika Taasisi ya Kibinafsi ya Andorra (BPA) hadi 2012. Mwaka huo alitumia fursa ya msamaha wa kodi ulioidhinishwa na serikali ya Uhispania kurekebisha fedha huko Andorra, sehemu nyingine yenye unafuu wa ulipaji kodi .

"Msamaha wa kodi ulikuwa wa kutatanisha kwa sababu uliwaruhusu wadanganyifu wengi kutakatisha fedha kwa gharama iliyopunguzwa," anaelezea Jesús García Bueno, mwandishi wa habari wa El País ambaye ni mtaalamu wa habari za kimahakama.

Kwa jumla, Guardiola alirekebisha hadi mfumo halali kiasi cha zaidi ya nusu milioni ya dola mwaka 2012 .Hadi wakati huo, mchezaji huyo wa zamani wa soka mwenye umri wa miaka 50 alikuwa hajatangaza pesa zozote alizokuwa nazo kwenye akaunti ya Andorra.

Lluis Orobitg, mwakilishi wa kocha huyo, alisema kwamba Guardiola alitumia tu akaunti ya Andorra kuingiza mshahara aliopokea kutoka kwa kilabu cha Qatar Al Ahli, ambapo alikuwa kati ya 2003 na 2005.

Julio Iglesias

Image: PARAS GRIFFIN / GETTY IMAGES

Kwa mujibu wa uchunguzi wa 'Pandora Papers', mwanamuziki huyo mwenye miaka 78, Julio Iglesias ana makampuni 20 kwenye visiwa vya Virgin: Makampuni 16, kwa jina la mkewe, Miranda Rijnsburger na mengine manne kwa jina lake.

Uchunguzi pia umeonesha kuwa msaniii huyo alitumia pesa iliyopatikana kutoka kwenye makampuni matano kununua majumba ya kifahari katika kijiji cha Indian Creek, kisiwa kilicho Miami, kinachofahamika kama ''bunker of the rich'' kwa kuwa eneo la kitajiri nchini Marekani.

Kwa mujibu wa data zilizotolewa na Pandora Papers kwa msaada wa kaunti ya Miami-Dade majumba hayo ya kifahari yanagharimu dola za kimarekani milioni 112.

Kadhalika, kwa mujibu wa uchunguzi, mwimbaji huyo alitumia fedha za makampuni mengine yaliyo nje kupata ndege binafsi na makampuni mengine sita kununua mali zenye thamani ya dola za kimarekani milioni nne.

Zote zinadhibitiwa na amana - taasisi inayokuruhusu kudhibiti mali zako nje ya nchi -, Julio Iglesias de la Cueva Revocable Trust, iliyoundwa mnamo 1995 katika Visiwa vya Virgin vya Uingereza.

Mwimbaji huyo hajazungumza lolote kuhusu hilo, lakini mnamo 2015 alimwambia mwandishi wa habari wa Uhispania Jordi Évole: "Sijawahi kuacha kulipa ushuru mkubwa mahali popote ulimwenguni; ambapo ninaimba, nalipa ushuru wangu."

Kwa mujibu wa mwakilishi wake, Juan Velasco, mwanamuziki huyo hakuwa na anuani ya ushuru nchini Uhispania tangu 1978.

Shakira

Image: KEVIN WINTER / GETTY IMAGES

Mwimbaji wa Colombia Shakira, 44, anamiliki kampuni tatu za nje zilizosajiliwa katika Visiwa vya Virgin vya Uingereza, kulingana na Pandora Papers: Light Productions Limited, Light Tours Limited, na Titania Management Inc.

Kampuni hizo tatu zilizinduliwa mnamo Aprili 2019, zikisimamiwa na kampuni ya mawakili ya Panama OMC, wakati Wizara ya Fedha ya Uhispania ikichunguza fedha zao.

Mwimbaji huyo aliyetamba sana na kibao machachari cha "Hips Dont lie", ambaye ameishi Barcelona (Uhispania) kwa miaka kumi, anakabiliwa na shutuma za udanganyifu wa ushuru unaofikia dola za Marekani milioni 16.83.

"Ukweli wa kuwa na kampuni nje ya nchi unategemea suala la kiutendaji na kibiashara, na kwa hali yoyote si kwa ajili ya kufurahia faida yoyote ya ushuru ", wanasema wawakilishi wao wa kisheria.

Miguel Bosé

Image: ANGEL MANZANO / GETTY IMAGES

Kulingana na Pandora Papers, mwanamuziki Miguel Bosé ameorodheshwa kwenye vyeti vya hisa vya 2016 vya kampuni ya nje iliyoundwa huko Uswizi, Dartley Finance, kupitia shirika binafsi la benki, Union Bancaire Privée (UBP) ya Geneva.

Wakati huo, mwimbaji aliishi Panama, ambapo alihamia mnamo 2014.

Kampuni ya Dartley iliundwa mnamo mwaka 2006 na inaendelea kufanya kazi. Kwa miaka kumi, lakini aina hii ya hati ilipigwa marufuku huko Panama mnamo 2015 kwa vitendo vyake vya kuficha mali.

Kampuni ya sheria inayosimamia kesi hiyo, Alemán Cordero Galindo y Lee (Alcogal), ingelilazimika kutoka mwaka huo kuwapa wanahisa "halisi" nyaraka zinazohusiana na kampuni hiyo. Jina la Miguel Bosé linaonekana tu tangu 2016, linaelezea gazeti la Uhispania "El País".

Elton John and Ringo Starr

Image: ,GETTY IMAGES / BBC WORLD

Mwanamuziki wa pop Elton John, 74, mmoja wa watetezi muhimu zaidi katika mapambano dhidi ya VVU / UKIMWI, ana zaidi ya kampuni 12 zilizosajiliwa katika Visiwa vya Virgin vya Uingereza, kulingana na uchunguzi.

Mumewe, David Furnish, ndiye mkurugenzi wa yote.

Mwanamuziki mwingine mashuhuri wa Uingereza, mpiga ngoma wa zamani wa Beatles Ringo Starr, 81, pia anaonekana kwenye Pandora Papers.

Richard Starkey (Ringo Starr) ameanzisha kampuni mbili katika visiwa vya Bahamas ambazo zilitumika kupata mali isiyohamishika, pamoja na "nyumba ya binafsi" huko Los Angeles.

Anahusishwa pia na amana tano za Panama: tatu kati yao ikiwa na bima ya maisha kwa watoto wake na nyingine ikiwa mapato kutoka kwa mrabaha na maonesho ya moja kwa moja.

Wawakilishi wa wasanii wa Uingereza hawakujibu maswali ya ICIJ.

Ángel Di María na Javier Mascherano

Image: GETTY IMAGES / BBC WORLD

Wanasoka wa Argentina Ángel Di María, 33, na Javier Mascherano, 37 ambaye sasa amestaafu, pia walipata mahali pa nafuu ya ushuru, kulingana na nyaraka za Pandora Papers, zilizopitiwa na La Nación, Infobae na elDiarioAR, washirika wa ICIJ huko Argentina.

Di María, ambaye kwa sasa anacheza Paris Saint-Germain, alianzisha kampuni huko Panama mnamo mwaka 2009, kifupi bila makao makuu au wafanyakazi wanaohusishwa na akaunti ya benki nchini Uswizi ambayo inasimamia mapato ya milionea huyo.

Sunpex Corporation Inc ilitoa mapato ya matangazo kutoka kwa bidhaa kama Adidas na Coca-Cola na uwekezaji uliosimamiwa kwa mali za kifedha. Ina mbia mmoja tu: Di María.

Di María alikiri mnamo 2017 kuwa ametenda kosa la ushuru mbele ya Hazina ya Uhispania kuhusu fedha zilizosimamiwa kupitia Sunpex kati ya 2011 na 2013, na kulipa faini ya zaidi ya dola za Kimarekani milioni 2.

Baada ya hukumu hiyo na kuondoka kwake Real Madrid, mwanasoka huyo aliendelea kusimamia mikataba ya matangazo kupitia kampuni hiyo ya nje, kulingana na uchunguzi.

"Kampuni hiyo imekuwa ikitangazwa England na Ufaransa. Ni mkakati wa kisheria kabisa," wawakilishi wao waliiambia ICIJ juu ya nchi ambazo di María amecheza tangu kuondoka kwake Uhispania.

Mazingira ya mchezaji huyo yalielezwa kwamba alitumia kampuni ya Panama kwa "pendekezo" lililotolewa na mhasibu wake mnamo 2009, na kwamba mchezaji wa mpira "hakujua kuwa pendekezo hili halikuwa la busara kwa mamlaka ya Uhispania."

Kwa upande mwingine, mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu wa Argentina Javier Mascherano, nahodha wa zamani wa timu ya Argentina na Barcelona, naye aliwekeza nje ya nchi, ripoti inasema.

Mwanasoka huyo alikuwa na ushirikiano kikampuni katika Visiwa vya Virgin vya Uingereza kati ya 2013 na 2016 ambapo alifanya uwekezaji wa mali isiyohamishika wakati akiishi Uhispania, kulingana na Pandora Papers.