Bidhaa tatu zilizopanda bei Kenya, Tanzania na Uganda

Image: BBC

Mafuta ya Petroli

Ongezeko hili limetokana na ongezeko la bei ya mafuta ghafi (crude oil) duniani katika miezi ya hivi karibuni, huku ulimwengu ukishuhudia ongezeko la shughuli za kiuchumi baada ya nchi nyingi kufungua biashara na kuonekana kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa corona kupitia chanjo na kanuni nyinginezo. Hali hii imepelekea hitaji la mafuta (demand) kuongezeka ikilinganishwa na uwepo wa mafuta yenyewe sokoni (supply).

Serikali za Tanzania na Kenya zimeweka mikakati ya kulinda umma dhidi ya bei za juu za mafuta, kupitia hatua kama vile kupunguza au kuondoa baadhi ya tozo na kodi kwa mafuta. Hata hivyo, bei ya mafuta bado iko juu ikilinganishwa na ilivyokuwa miezi michache iliyopita. Tuangalie hali ilivyo katika nchi zenyewe:

Image: GETTY IMAGES

Tanzania: Mwezi Novemba, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilitangaza bei mpya za petroli kuwa TZS 2,439 ($1.06) kwa lita, na TZS 2,243 ($0.97) kwa lita ya dizeli mjini Dar es Salaam. Mnamo Septemba, bei ya lita moja ya petroli ilikuwa Tsh 2511 ($1.09), huku dizeli ikiuzwa 2291 ($1.00) kwa lita mjini Dar Es Salaam.

Kenya: Taifa hili hutangaza bei mpya za mafuta ya petroli mnamo tarehe 14 ya kila mwezi. Mnamo Oktoba na Novemba (2021), bei za mafuta hazijabadilika. Mjini Nairobi, bei ya lita moja ya petroli ni Ksh129.72 ($1.16), huku diesel ikiuzwa Ksh110.6 ($0.98) kwa lita. Kenya ilishuhudia ongezeko kubwa zaidi la bei ya mafuta mnamo Septemba, ambapo bei ya lita moja ya petroli ilikuwa Ksh 134.72 ($1.20), huku dizeli ikiuzwa Ksh 115 ($1.02) kwa lita. Ongezeko la bei ya mafuta nchini Kenya imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kodi ambazo zinatozwa bidhaa hiyo.

Uganda: Bei ya mafuta imeongezeka kwa wastani wa UGX 500 ($0.14) kwa lita katika wiki chache zilizopita, na sasa bei ya lita moja ya petroli ni UGX 4600 ($1.28) mjini Kampala huku dizeli ikiwa UGX 4200 ($1.17). Mwezi Juni, bei ya lita moja ya petroli ilikuwa UGX 3900 ($1.09), huku dizeli ikiwa UGX 3500 $0.98) mjini Kampala.

Mafuta ya kupikia

Image: GETTY IMAGES

Mafuta ya kupikia yameshuhudia ongezeko la bei. Nchini Uganda, bei ya lita moja ya mafuta imeongezeka kutoka UGX 5000 ($1.40) hadi UGX 8,000 ($2.23) mwezi huu, kulingana na bodi ya takwimu nchini humo UBOS. Kwa jumla, bei ya siagi (margarine) na mafuta mengine ya kula imeongezeka kwa wastani wa UGX 2000 ($0.56).

Nchini Kenya, bei ya mafuta ya kupikia yameongezeka kutoka Ksh 250 ($2.23) kwa lita kwa jumla mwezi Oktoba hadi Ksh 300 ($2.67) kwa lita mwezi Novemba.

Nchini Tanzania, bei ya lita moja ya mafuta ya kupikia ni TZS 7,600 ($3.3), huku lita tano za mafuta hayo zikiuzwa kwa TZS 38000 ($16.51) kwa wastani. Bei hii inatofautiana na bidhaa za mafuta za kampuni tofauti.

Bei ya mafuta haya ambayo hutumiwa kupikia vyakula vingi imepanda kutokana na upungufu wa bidhaa hiyo duniani ikilinganishwa na hitaji lililopo (low supply, high demand), na hali hii imechangia katika kuongezeka kwa mfumuko wa bei za bidhaa za chakula.

Bidhaa za chakula

Bei ya bidhaa za chakula imeongezeka kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo mfumuko wa bei, kushuka thamani kwa sarafu za nchi husika dhidi ya dola, ukosefu wa mvua ya kutosha, na kodi au tozo.

Nchi zote tatu - Kenya, Uganda na Tanzania zimekuwa zikishuhudia viwango tofauti vya mfumuko wa bei, ambao umechangia ongezeko la baadhi ya bidhaa za chakula.

Nchini Uganda, bei za bidhaa zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 10% mwezi huu, kulingana na bodi ya tawimu UBOS. Hali hii imesababisha bidhaa za matumizi ya nyumbani kama vile sabuni ya kuoga, na pia chakula kuongezeka.

Image: HABARI LEO

"Uganda ni nchi yenye mazingira mazuri ya kilimo, na utapata kwamba bei ya chakula hulingana na soko, na bei yenyewe pia hutathminiwa katika masoko tofauti. Kwa mfano, tulikuwa tunanunua kibunda/kifurushi cha matooke (ndizi) kwa bei ya UGX 20,000, lakini sasa tunanunua kwa UGX 30,000 na saa zingine hata zaidi ya hiyo bei," alisema mkaazi mmoja wa Kampala ambaye hakutaka kutambuliwa.

Nchini Kenya, mfumuko wa bei mwezi Septemba ulifikia asilimia 6.91%, na kisha ukapungua hadi 6.45% mnamo Oktoba kulingana na bodi ya takwimu KNBS. Kujaza mtungi (refilling) wa kilo 13 wa gesi ya kupikia LPG sasa inawagharimu wananchi Ksh 3,000 ($26.7) kutokana na tozo la asilimia 16% ambalo ni kodi ya VAT.

Nchini Tanzania, mfumuko wa bei uliongezeka hadi kufikia asilimia 4% mwezi Septemba, kutoka asilimia 3.8% mnamo Agosti. Ongezeko hili lilitokana na ongezeko la bei za bidhaa kama vile unga wa ngano, ambao uliongezeka kwa asilimia 6.8% huku bei ya nyama ya ng'ombe ikiongezeka kwa asilimia 3.4% kwa mujibu wa bodi ya kutoa takwimu NBS. Bidhaa zingine ambazo zimeshuhudia kuongezeka kwa bei nchini humo ni vifaa vya ujenzi, tozo za kutuma au kupokea pesa kupitia miamala, na luku (malipo ya umeme).

Mchumi Walter Nguma anasema kwamba huenda hali ya uchumi ikaendelea kuwa hivi kwa muda.

"Sioni dalili ya bei ya bidhaa kushuka, kwasababu hali ya uchumi haijawa vizuri kabisa. Ukigusa petroli, mafuta ya kupikia na miamala, moja kwa moja hauwezi ukazuia mfumuko wa bei, lazima utaongezeka. Kitakachoweza kupunguza bei ni pale ambapo miamala hii itapunguzwa na gharama ya mafuta kushuka," anasema Walter.