Fahamu shughuli za kustaajabisha ambazo vijana nchini hujihusisha nazo ili kujikimu kifedha

Muhtasari

•Matokeo ya sensa iliyofanyika nchini mwaka wa 2019 yaliashiria kuwa zaidi ya theluthi ya vijana wa hapa nchini ambao wamehitimu kuwa na kazi hawana kazi.

Pesa za Kenya
Pesa za Kenya
Image: HISANI

Suala la kukosa kazi haswa kwa vijana limekuwa suala nyeti sana nchini kwa miaka mingi.

Matokeo ya sensa iliyofanyika nchini mwaka wa 2019 yaliashiria kuwa zaidi ya theluthi ya vijana wa hapa nchini ambao wamehitimu kuwa na kazi hawana kazi.

Vijana wanapohitimu umri wa miaka 18 hushinikizwa kujitegemea kwa mambo mbalimbali hata wakiwa bado wanaishi kwa wazazi wao.

Suala la kukosa kazi limewashinikiza  vijana wengi kujihusisha na shughuli nyingi, zingine sawa na zingine za kustaajabisha katika juhudi za kujaribu kujikimu kifedha.

Hizi hapa baadhi ya shughuli hizo;-

  1. Uandishi wa kimitandao (Online writing)

Hii ni mojawapo ya shughuli ya kutengeneza pesa maarufu sana miongoni mwa vijana haswa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Anachohitaji kuanza kazi ile ni kipakatalishi (Kompyuta), data za kimitandao au WiFi na kujuana na watu ambao wako katika nafasi ya kumuunganisha na kazi zile.

Mapema mwaka huu stesheni moja ya runinga Marekani ilifichua kuwa kunao vijana wengi nchini Kenya ambao wanasaidia wanafunzi kutoka Marekani kufanya kazi zao za shule kwa malipo.

Mazungumzo yote na malipo hufanywa kwa njia ya kimitandao.

  1. Mahusiano ya kimapenzi na watu tajiri wenye umri mkubwa (Sponsors)

Hamu ya pesa imewashinikiza maelfu ya vijana nchini kuwa na mahusiano wa kimapenzi na watu waliowazidia umri, almuradi wana pesa.

Vijana hao hukubali kuhusiana na wazee hao wanaofahamika zaidi kwa jina la kitani kama 'sponsors' ili kupata manufaa ya kifedha.

Kuna baadhi yao ambao huchumbia 'sponsors' ili waweze kulipa bili zao, kunao wanaojiingiza kwenye mahusiano yale ili waweze kununuliwa vitu wanavyohitaji na kunao wanaofanya vile ili mradi watajirike kwa haraka.

Jambo hilo halihusishi vijana wa kike tu mbali hata wa kiume wamejitosa kwenye biashara ile. Wengi wao hawaangazii umri ila mfuko wa 'sponsors' wao.

Night club
Night club
Image: HISANI
  1. Kucheza densi

Kwa kawaida kucheza densi ni shughuli ya kujiburudisha ila kwa wengine densi ni kazi ambayo inawaletea mapato.

Kuna watu wengi haswa vijana ambao wanatumia talanta zao za kucheza densi kutengenezea pesa. 

Wacheza densi hulipwa kwa kushirikishwa kwa video ya ngoma (Vixens), kutumbuiza wateja kwa klabu na kutumbuiza wageni kwa sherehe n.k.

Wengine hujitolea kucheza densi wakiwa uchi ama nusu uchi mradi tu waweze kulipwa.(strippers)

  1. Kucheza kamari (Betting)

Kamari almaarufu kwa kiingereza kama 'Betting' ni moja ya shughuli ambayo vijana wengi wamejitosa ndani yake.

Kwa uhalisi mchezo wa kamari sio kazi ila vijana wengi wameichukulia kama biashara na wanawekeza maelfu ya pesa wakiwa na matumaini ya kutengeneza pesa zaidi.

Kunao ambao hubahatika kushinda ila kuna wengi wao ambao hupoteza pesa nyingi mno kwenye harakati ya kucheza kamari.

Michezo ya kamari huwa tofauti kuanzia kwa ubashiri wa soka, mbio za magari, riadha kati ya zingine.

Nchini Kenya kunazo kampuni nyingi ambazo hutoa huduma za mchezo wa kamari na asilimia kubwa ya vijana wamezama kwenye uraibu wa michezo hiyo.

  1. Ufadhili wa mbegu za uzazi.
Mbegu ya kiume
Mbegu ya kiume
Image: HISANI

Hamu ya kupata fedha pia imewafanya baadhi ya vijana wenye umri wa miaka  20-30 kujihusisha na shughuli ya ufadhili wa mbegu za kiume. Hii ni shughuli ya kawaida ambayo inaendelea nchini kwa ufiche .

Wanawake ambao hawana wachumba na wanatamani kupata watoto ndio wateja wakuu wa vijana hao.

Pia kunao wanandoa ambao hawana uwezo wa kupata watoto kwa pamoja na hulipia huduma za vijana hao kusaidia kutatua tatizo lao.

Kunao wanawake ambao hujitolea kubeba ujauzito kwa niaba ya wanandoa kwa malipo.