Fahamu mambo 10 yanayofanywa na wanaume ambayo huwakera sana wanawake

Muhtasari

•Kama ilivyo asili yake, vipo ambavyo utavipenda kutoka kwa mwenza wako na vipo ambavyo utavichukia ama havitakufurahisha.

Image: ALAMY

Binadamu amekuwa na vitu vyake anavyovipenda sana na vingine kuvichukia sana. Vipo anavyovipenda kidogo na vingine anavichukia kidogo, lakini vipo ambavyo hajui kama anavipenda ama anavichukia.

Na kupenda kitu ama kukichukia kitu ni asili ya binadamu ingawa vipo baadhi ya vitu ambavyo anaweza kuvipenda ama kuvichukia kutokana na vichocheo vya kimazingira.

Wanawake pia kama sehemu ya binadamu hao, pia wana vitu wanavyovipenda na kuvichukia.

Ukiwa katika uhusiano unaweza kuviona vitu vingi zaidi kutoka kwa mwenza wako. Kama ilivyo asili yake, vipo ambavyo utavipenda kutoka kwa mwenza wako na vipo ambavyo utavichukia ama havitakufurahisha.

Kwa mujibu wa mtandao wa Danburycountry vitu vingine unaweza kuviona mwanzoni kabisa mwa uhusiano wako au hata kabla ya kuanza uhusiano huo, vingine vinaonekana wakati wa mahusiano yakiendelea na vingine vikaonekana hata baada ya mahusiano kwisha.

Ukiacha vitu vingine vinavyoweza kupimika na kuonekana kwa mazingira ulipo, vipo vitu ama mambo ambayo hufanywa na wanaume ambayo huwachukiza na kuwakera sana wanawake.

Miongoni mwa vitu hivyo ni hivi 10

1O: Kuangalia mpira ama michezo

Image: GETTY IMAGES

Wanaume wanapenda sana mpira. Kama kuna kitu ambacho kinawaleta pamoja na kuwakusanya wanaume ni michezo hasa soka. Hata kama kuna mwanamke anapenda kutazama michezo, mwanaume yuko radhi ambebe mwanaume mwenzake kwenda kutazama mechi uwanjani ama kutazama pamoja kwenye Televisheni wakiwa baa, kwenye migahawa ama nyumbani.

Wakiwa Pamoja watapiga makelele, watabishana, kuna wakati watazungumza mpaka lugha chafu kwa utani. Siku ya mechi, kinachothaminiwa sana na mwanaume wakati huo ni mechi inayochezwa. Muda wa mwanaume utatumika zaidi katika mchezo huo kuliko kuutumia kwa ajili ya mwanamke.

Wanawake hujihisi kama kutengwa, kutothaminiwa…na hudhani kama si sehemu ya maisha ya wanaume wakati wenza wao ama marafiki zao wa kiume wakiwa wanatazama mpira.

9: Kumuangalia mwanamke mwingine

Kumuangalia mwanamke mwingine
Kumuangalia mwanamke mwingine
Image: GETTY IMAGES

Jambo hili linaelezwa liko kwenye asili ya mwanaume, kama sehemu ya vinasaba vyake, ni kitu ambacho kiko nje ya uwezo wake. Haijalishi ana furaha kiasi gani katika mahusiano yake, atakapomuona mwanamke mzuri ama mrembo kwa vipimo vya macho yake akipita mbele yake ama popote, atamuangalia.

Sasa inategemea mwanaume huyo amemuangalia kwa muda gani na hisia gani kwa namna atakavyotafsiriwa na mwenza wake. Wanaume wengine hujikaza na kutogeuka wanapokuwa wameambatana na wenza wao, ingawa kwa sekunde hata moja kwa jicho la kuibia, alipata wasaa wa kumuangaia mwanamke huyo mzuri na wa kuvutia kwake'. Jambo hili kwa wanawake wengi hawalipendi. Hawapendi waume ama wenza wao wawaangalia hasa kwa jicho la tofauti wanawake wengine.

8: Kutofanya kazi za nyumbani

Kama uko kwenye mahusiano ni jambo muhimu kushirikiana kwenye majukumu mbalimbali kwa mfano, usafi, kufua, hata kupika. Kama wewe ni mwanaume na unafanya haya mwanamke uliye naye hatakuwa na shida na wewe, huenda akaongeza mapenzi zaidi kwako, lakini ukifanya tofauti, pengine hatoacha kukupenda ila hatopenda unachokifanya.

7: Kutomsikiliza mwanamke

Dhana kubwa hapa ni kwamba mwanamke anaongea, mwanaume anasikiliza. Lakini kwa bahati mbaya hilo haliwezekani wakati wote. Inategemea masuala anayozungumza mwanamke na namna mwanaume anavyopokea. Haijalishi jambo linalozungumza lina umuhimu kiasi gani, kwa namna baadhi ya wanawake wanavyoliwasilisha, wanaume hupokea machache na kuyafanyia kazi. Ni jambo la kibinadamu linalowakera.

Mwanamke akirejelea jambo zaidi ya mara tatu kulisema na mwanaume hajalifanyia kazi, wanawake wengi huwa hawapendezwi.

6: Kutomfanyia vitu vya kumshangaza

Hakuna kitu kinachomfanya mwanamke kufurahia kama kumfanyia vitu vya kumshangaza tena kwa kumshitukiza. Bila kujua ama kutarajia unamnunulia kitu anachokipenda na kumpelekea ama unamfanyia kitu ambacho hakudhania kama kingeweza kufanyika. Inaweza kuonekana ni jambo dogo sana lakini ni muhimu kwao, na kwako kukufanya uendelee kuwa kwenye himaya ya kukuthamini.

5: Kukoroma usingizini

Mwanamke aliyechoka na kelele za kukoroma za mumewe usiku
Mwanamke aliyechoka na kelele za kukoroma za mumewe usiku
Image: GETTY IMAGES

Jambo hili ni tata, na linahusu asili na wakati mwingine maumbile ya mtu. Japo inafanyika, lakini kujizuia kukoroma ni sayansi ngumu kwa walio wengi. Ingawa ni wazi wanawake na wao wanakoroma pia, lakini ni wanaume wanaoathirika zaidi na uamuzi wa kuchukia tendo hilo kwa sababu wanawake wengi hawapendi kuona mtu akikoroma.

4: Kukataa kufanya kazi zaidi ya moja 

Sio kwamba wanaume hawawezi kufanya kazi zaidi ya moja kwa wakati mmoja, ni kwa sababu mwanaume asili yake, akianza kufanya kazi moja huwa anafanya kazi hiyo kwa akili yake yote. Kujigawa kwake ni mtihani hasa kwa kazi za kawaida. Kwa aslimia 100% hujielekeza kwa kazi iliyo mbele yake, akimaliza anaanza kazi nyingine.

Wanawake wana uwezo wa kufanya kazi zaidi ya moja kwa wakati mmoja, anaweza akawa anapika, huku anafua, wakati huo huo akiwa na mtoto mgongoni.

Mwanaume mpaka amalize moja aanze nyingine. Tatizo linaanza kama mwanamke atakuwa anamtaka mwenza wake afanya kama yeye. Lakini inawezekana mwanaume kufanya hivyo kwa kutenga muda wa kufanya hayo kwa ufanisi.

3: Kutoa hewa chafu hadharani

Wanaume wengi kwa asili ni watu wasio na aibu kulinganisha na wanawake. Mwanamue anaweza kupumua hadharani akiwa na wenzake, lakini mwanamke hata kukiri tu kwamba aliwahi kufanyahivyo hawezi, kwa sababu ya haiba ya aibu aliyoumbwa nayo.

Wanawake wengi hawapendi kumuona ama kumsikia mwanaume ambaye anafanya hivyo hadharani, ama kwa bahati mbaya ama kwa makusudi.

2: Kuhodhi rimoti ya TV

Image: GETTY IMAGES/ YVAN COHEN

Hili ni jambo dogo kwa jicho la mbali, lakini kubwa kwa mwanamke. Wanawake hupenda kuangalia vitu vingi kwenye Televisheni, vingine vinaweza kuonekana havina mvuto kwa mwanaume. Vitu kama mapishi, urembo na tamthilia. Mwanaume mara nyingi hujiona anastahili kuangalia masuala yake kama mpira na filamu za kutisha. Hapo ndipo matatizo yanapoanzia kwa mwanaume, na mwanamke kukunja sura kila mwanamke anapokaa kitandani ama sebuleni kuangalia Televisheni.

1: Kutokiri makosa

Kusema nimekosea, ni kitu kigumu kwa baadhi ya wanaume, hata kama wamekosea kweli. Wapo wanaodhani kwamba wakisema wamekosea ama wakikiri makosa mbele ya wenza wao, ni sawa na kusema mie mdhaifu nimeshindwa. Kwa lugha nyingine, mwanaume hataki kuonekana mdhaifu, lakini kukiri kosa sio udhaifu, na wanawake hujiona wenye nafasi pale kosa linapoonekana kila mmoja kukiri.