Kijana wa miaka 25 apanga kuoa ajuza wa 85, aapa kujitia kitanzi mkewe akifariki kabla yake

Muhtasari

•Muima ,25,  ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu amesema yupo tayari kufunga pingu za maisha na Thereza ,85, ambaye ni mmiliki manyumba za kupanga.

•Muima alifichua kwamba Thereza alianza kumtunza vizuri na kumsaidia kwa chakula na fedha na hapo ndipo akaanza kumpenda.

•Thereza alifichua kwamba watoto wake wamemwagiza Muima alipe mahari ya ng'ombe kumi na wawili ili harusi ifanyike.

Muima na Mpenzi wake Thereza
Muima na Mpenzi wake Thereza
Image: SCREEN GRAB// AFRIMAX

Jamaa mmoja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amewashangaza wengi kutokana na uamuzi wake wa kufunga ndoa na mwanamke aliyemzidia umri kwa miaka 60.

Muima ,25,  ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu amesema yupo tayari kufunga pingu za maisha na Thereza ,85, ambaye ni mmiliki manyumba za kupanga.

Wakiwa kwenye mahojiano na Afrimax, Muima alisema walijuana baada yake kukodi mojawapo wa nyumba ambazo Thereza anamiliki.

"Namna alivyokuwa ananitendea ilinisukuma kumpenda. Hata kama yeye ni mwanamke mzee na kusema kweli yeye ni kama nyanya yangu, nampenda," Muima alisema.

Muima alifichua kwamba Thereza alianza kumtunza vizuri na kumsaidia kwa chakula na fedha na hapo ndipo akaanza kumpenda.

Amesisitiza kwamba ni chaguo lake kumpenda ajuza huyo ambaye ana watoto wanane wakubwa na wajukuu ishirini.

"Hili ni chaguo langu na ni furaha yangu. Kila mtu ana kinachomfurahisha. Kabla ya kufurahisha wengine, hakikisha kwamba umejifurahisha mwenyewe. Siyatilii maanani maoni ya watu," Muima alisema.

Thereza kwa upande wake alisema yupo tayari kuvishwa pete na kijana huyo mwenye umri sawa na mjukuu wake wa tano.

Alifichua kwamba watoto wake wamemwagiza Muima alipe mahari ya ng'ombe kumi na wawili ili harusi ifanyike.

"Yeye yuko tayari kulipa. Tunapendana," Thereza alisema

Muima alifichua kwamba hapo awali aliwahi kujaribu mahusiano na wanadada wenye umri  wa ujana ila wakamhangaisha sana hadi akafikia kufanya maamuzi ya kuachana nao.

"Sitachagua msichana mwingine ila huyo (Thereza). Naomba asifariki mbele yangu kwani naweza kujitia kitanzi mara moja," Muima alisema.

Wawili hao walisema ndoa yao imekabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa familia, marafiki na jamii. Hata hivyo wameshikilia msimamo wao kwamba wanapendana na wanakusudia kuishi pamoja hadi kifo.