Fahamu hatua za Harusi ya Kitamaduni ya Wakikuyu

Hivi majuzi, Wakenya wamekuwa wakichagua kufunga ndoa katika harusi za kitamaduni.

Muhtasari

•Kuhanda ithigi ni hatua ya kwanza ya harusi ya kitamaduni ya Wakikuyu. 

•Baada ya bwana na bibi harusi kukata bega pamoja basi wanaweza kutambuliwa kama mke na mume.

Pete
Pete
Image: SERENDIPITY DIAMONDS

Katika miaka ya hivi majuzi, Wakenya wengi wakiwemo watu mashuhuri wamekuwa wakichagua kufunga pingu za maisha katika harusi za kitamaduni kulingana na mila na desturi za jamii walizotokea.

Hili limekuwa jambo ambalo limekuwa likivuma miongoni mwa jamii nyingi huku Wakenya wakijaribu kufufua baadhi ya tamaduni zilizosahaulika. Jamii ya Wakikuyu imekuwa hai sana  katika hili katika siku za hivi karibuni.

Katika makala haya tunaangazia hatua za harusi ya Kitamaduni miongoni mwa jamii ya Kikuyu:-

i) Kuhanda ithigi

Kuhanda ithigi ni hatua ya kwanza ya harusi ya kitamaduni ya Wakikuyu. Tambiko hili kimsingi humaanisha ‘kujiandikisha.’

Bwana harusi mtarajiwa huenda kwa kina bi harusi pamoja na baadhi ya wanafamilia na wazee waliochaguliwa ili kuwajulisha wazazi wa bibi-harusi kuhusu nia yao ya kumwoa binti yao.

Baada ya mwanamume kuwashawishi wazazi wa bibi-harusi kuhusu nia yake na wakawa wameridhika, basi bibi arusi anahifadhiwa kwa ajili yake.

Baada ya hatua hii wazazi wa bibi harusi hawawezi kuchukua posa zingine zozote kwa ajili ya binti yao. Hii ni kwa sababu tayari ‘ameandikishwa’ kwa ajili ya ndoa.

ii) Njohi ya njurio

Njohi kwa Kikuyu inamaanisha bia. Njurio maana yake ni kuuliza.

Hatua hii ya pili ya harusi ya kitamaduni ya Kikuyu kimsingi inahusisha upande wa bwana harusi kutembelea upande wa bi harusi ili kuuliza kuhusu matakwa yao kwa ajili ya binti yao.

Katika hatua hii, wawakilishi kutoka pande zote mbili hukunywa bia ya kitamaduni (muratina) pamoja huku wakiendelea kujadiliana.

Upande wa bibi harusi hufahamisha upande wa bwana harusi jinsi ambavyo huwa ‘wanauza’ binti zao.

Pia wao huorodhesha madai yote wanayofanya kwa kawaida ili kumwachilia binti yao kwa ndoa.

NB: Upande wa bwana harusi hauruhusi kujitetea katika hatua hii.

iii) Ruracio

Ruracio ni hatua ya malipo ya mahari.

Hatua hii inaweza kufanywa kwa awamu, kulingana na mahitaji ya upande wa bibi harusi na uwezo wa upande wa bwana harusi kuzitimiza.

Upande wa bwana harusi hufanya ziara nyumbani kwa kina bibi harusi. Upande wa bibi harusi huwakaribisha wakwe zao kulingana na mila zao. Familia tofauti zina njia tofauti za kuwakaribisha wakwe.

Baada ya wakwe kukaribishwa, utambulisho hufanywa kwa pande zote mbili kabla ya bibi harusi kutolewa nje.

Kitamaduni, bi harusi mara nyingi hutolewa nje pamoja na wanawake wengine walio na sifa karibu sawa na yeye, ambao wote kwa kawaida huwa wamefunikwa na leso kutoka kichwa hadi miguu. Hii huwa mtihani kwa bwana harusi kuona kama anaweza kumtambua mkewe kwa urahisi .

Baada ya bwana harusi kufanikiwa kumtambua mkewe, wawakilishi kutoka upande wake huelekezwa kwenye chumba ili kushiriki mkutano na wawakilishi kutoka upande wa bibi arusi.

Matakwa husmowa tena na katika hatua hii upande wa bwana harusi unaweza kujietea. Ikiwa upande wa bwana harusi una uwezo wa kulipa madai yote, basi wanaendelea na kuifanya. Wanaweza pia kuchagua kulipa katika tarehe ya baadaye.

iv) Ngurario/Kurenga kiande

Hii ndiyo hatua ya mwisho ya harusi ya Kikuyu. Taratibu kadhaa hufanyika katika hatua hii.

Kondoo mkubwa na mwenye afya anayejulikana kama ‘ngoima’ huchinjwa mbele ya familia zote mbili na wageni.

Kurenga kiande maana yake ni kukata bega. Wanandoa huchukua kisu na kukata bega la kondoo pamoja.

Baada ya wote wawili kukata bega pamoja basi wanaweza kutambuliwa kama mke na mume. Kisha bibi-harusi hupatiwa masikio, ulimi na figo ya kondoo huyo kula.

Masikio huwa ishara kwamba mwanamke anapaswa kuwa tayari kila wakati kumsikiliza mume. Ulimi unaashiria kwamba mwanamke anapaswa kuwa mwangalifu kwa kile anachosema na jinsi anavyozungumza na mume.

Kisha bibi harusi hupewa bakuli la uji ili kumlisha mume.

Wanandoa na wageni kisha hushereehekea pamoja kwa shangwe na nderemo.

Imekuwa ada kwa Wakikuyu  kuvaa mavazi ya kahawia katika hatua hii ya mwisho ya harusi.