Jinsi kuku unayemla ulivyokua kwa 400% kwa miaka 50

Image: BBC

Nia ilikuwa kuzalisha kuku wakubwa wa nyama na wenye uwezo wa kulisha familia nzima kwa gharama ya chini.

Mnamo 1946, mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, serikali ya Marekani iliungana na kampuni kuanzisha shindano ambalo lilibadilisha milile ufugaji wa kuku duniani.

Shindano la Chicken of tomorrow liliwaleta pamoja wakulima na wafugaji kutoka kote nchini kuendeleza mpango huo kwa kuzingatia uteuzi wa vinasaba, kuku wa nyama wenye uwezo wa kukua haraka huku wakiwa na nyama bora zaidi.

"Kwa ushindani, walitaka kuzalisha ndege ambao wangeweza kupata misuli haraka na ambao wangeweza kuchinjwa katika umri mdogo," Richard Thomas, mtaalam wa akiolojia ya ndege katika Chuo Kikuu cha Leicester, Uingereza, alielezea BBC Mundo.

Nchi ya Amerika Kaskazini ilitaka kukidhi mahitaji makubwa ya protini kama matokeo ya ongezeko la idadi ya watu wakati huo.

Kando na hilo, vita hivyo vilisababisha nyama nyekundu kutolewa kwa mgao kama hatua ya ambayo ilikusudiwa kuwalisha askari waliokuwa vitani.

Lakini wakati huo, kuku alikuwa mnyama ndege mdogo, aliyefugwa zaidi kwa ajili ya mayai na alichukua muda wa miezi minne kukua.

Katika zaidi ya nusu karne, kulingana na utafiti wa Chuo Kikuu cha Alberta uliochapishwa mwaka wa 2014, wastani wa ukubwa wa kuku wa nyama umeongezeka kwa 400%.

Martin Zuidhof, mmoja wa waandishi wa utafiti huo, alithibitisha kwamba kile kilichotokea katika ushindani huo kilishawishi ukubwa kuku tunayemla leo.

"Ndoto ya Marekani ilikuwa ya kila familia kupata kitoweo, kwa kila mtu kuwa na furaha. Hiyo ilikuwa sababu [ya kukuza kuku]," daktari katika Sayansi ya Wanyama alisema.

"Ilikuwa na shindano hili katika miaka ya 1940 ambapo kuku wa kwanza wa nyama au kuku wa viwandani, kwa kusema, walitolewa," Profesa Thomas anaiambia BBC Mundo.

Sasa Zuidhof, anasema mnyama huyu, anaweza kuchinjwa katika kipindi cha wiki 4 au 5 ikilinganishwa na miezi minne kabla ya shindano hilo.

Na bei yake, kulingana na nakala katika gazeti la The Economist, ilishuka kwa 47% kutoka 1960 hadi 2019.

Kwa sasa, bei ya kuku nchini Marekani ni dola za Marekani 1.92 kwa pauni (nusu kilo), wakati miaka 59 iliyopita ilikuwa na thamani ya sawa na dola za Marekani 3.63 (iliyorekebishwa kwa mfumuko wa bei).

Shindano hilo, pamoja na mbinu za uzalishaji viwandani na maendeleo ya kiteknolojia yaliyofuata, yalisaidia kubadilisha nyama hii kuwa bidhaa inayoweza kufikiwa na mamilioni ya watu.

Harakati ya kutafuta nyama "bora".

Makala maalum yaliyotayarishwa mwaka wa 1948, yalitumiwa kutangaza Shindano la Kuku wa Kesho na yalitoa maelezo shindano hilo hatua kwa hatua, ikuashiria kuwa kuku "bora" anapaswa kuwa yule "akichinjwa" ana asilimia kubwa ya nyama ya kifua na mapaja

"Kuku mwenye sifa bora za nyama nyeupe", anasikika akisema mwigizaji maarufu Lowell Thomas, ambaye aliwahi kuwa mtangazaji.

Ili kuwapa motisha wafugaji na wafugaji wa kuku, kampuni ya A & P, muuzaji mkuu wa Marekani wakati huo, ilitoa dola 10,000 za Kimarekani kama zawadi kwa washindi wa shindano hilo.

Mashindano hayo ambayo yaliandaliwa na kamati iliyoongozwa na Idara ya Kilimo ya Marekani, yalianza kwanza katika ngazi ya serikali na kuishia katika ngazi ya kitaifa.