Homa ya Mgunda: Ufahamu ugonjwa huu uliobainika kusini mwa Tanzania

Leptospirosis ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria unaoathiri wanadamu na wanyama.

Muhtasari

•Serikali ya Tanzania imebaini kuwa ugonjwa unaoua watu kusini mwa Tanzania ni homa ya Mgunda.

•Bakteria wanaosababisha leptospirosis huenezwa kupitia mkojo wa wanyama walioambukizwa, ambao wanaweza kuingia ndani ya maji au udongo na wanaweza kuishi huko kwa wiki hadi miezi.

Image: BBC

Serikali ya Tanzania imebaini kuwa ugonjwa unaoua watu kusini mwa Tanzania ni homa ya Mgunda.

Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amewaambia waandishi wa habari kuwa upimaji wa sampuli za wagonjwa waliokuwa wakiugua katika Wilaya ya Ruangwa katika Mkoa wa Lindi umethibitisha mlipuko huu kuwa wa ugonjwa unaoitwa kitalaamu Leptospirosis, Field Fever au kwa lugha ya Kiswahili inajulikana kama Homa ya Mgunda.

Homa ya Mgunda au Leptospirosis ni nini?

Leptospirosis ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria unaoathiri wanadamu na wanyama.

Husababishwa na bakteria kitaalamu kutoka jenasi ya Leptospira. Kwa wanadamu, inaweza kusababisha dalili nyingi, ambazo nyingine zinaweza kudhaniwa kuwa magonjwa mengine.

Baadhi ya watu walioambukizwa, hata hivyo, wanaweza wasiwe na dalili zozote.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kupambana na magonjwa CDC, bila matibabu, inaweza kusababisha uharibifu wa figo, meningitis (kuvimba kwa membrane karibu na ubongo na uti wa mgongo), kwa ini kushindwa kufanya kazi , shida ya kupumua, na hata kifo.

Ugonjwa huu huambukizwa vipi?

Bakteria wanaosababisha leptospirosis huenezwa kupitia mkojo wa wanyama walioambukizwa, ambao wanaweza kuingia ndani ya maji au udongo na wanaweza kuishi huko kwa wiki hadi miezi.

Aina nyingi tofauti za wanyama wa porini na wa nyumbani hubeba bakteria.

Halikadhalika Ng'ombe, Nguruwe, farasi, mbwa, jamii ya panya na wanyama wa porini.

Wakati wanyama hawa wakipata maambukizi, wanaweza kuwa hawana dalili za ugonjwa huo. Wanyama walioambukizwa wanaweza kuendelea kutoa bakteria kwenye mazingira kwa kuendelea au kila baada ya muda kwa miezi michache hadi miaka kadhaa.

Mwanadamu anaweza kuambukizwa kupitia:

  • Kugusa mkojo au maji mengine ya mwili (isipokuwa mate) kutoka kwa wanyama walioambukizwa.
  • Kugusa maji, udongo, au chakula kilichochafuliwa na mkojo wa wanyama walioambukizwa.

Bakteria wanaweza kuingia mwilini kupitia ngozi au utando wa (macho, pua au mdomo), hasa ikiwa ngozi ina mikwaruzo.

Kunywa maji machafu pia kunaweza kusababisha maambukizi.

Milipuko ya leptospirosis kwa kawaida husababishwa na maji machafu, kama vile maji ya mafuriko. Maambukizi ya mtu kwa mtu ni nadra.

Dalili za homa ya Mgunda

Kwa wanadamu, inaweza kusababisha dalili mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:

  • Homa kali
  • Maumivu ya kichwa
  • Baridi
  • Maumivu ya misuli
  • Kutapika
  • Jaundice (ngozi ya manjano na macho)
  • Macho mekundu
  • Maumivu ya tumbo
  • Kuhara
  • Upele

Dalili nyingi hizi zinaweza kuhusishwa na magonjwa mengine.

Isitoshe, baadhi ya watu walioambukizwa huenda wasiwe na dalili zozote.

Kwa mujibu wa CDC, Muda kati ya kufichuliwa kwa mtu kwa chanzo kilichochafuliwa na kuwa mgonjwa ni siku 2 hadi wiki 4.

Ugonjwa kawaida huanza ghafla na homa na dalili nyingine. Leptospirosis inaweza kutokea katika hatua mbili:

Baada ya awamu ya kwanza (pamoja na homa, baridi, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, kutapika, au kuhara) mgonjwa anaweza kupona kwa muda lakini akawa mgonjwa tena.

Awamu ya pili ikitokea, huwa ni kali zaidi; mtu anaweza kupata shida ya figo au ini au homa ya uti wa mgongo.

Ugonjwa hudumu kutoka siku chache hadi wiki 3 au zaidi.

Bila matibabu, kupona kunaweza kuchukua miezi kadhaa.

Ni watu gani wako katika hatari ya kupata maambukizi?

Leptospirosis hutokea duniani kote, lakini ni kawaida zaidi katika hali ya hewa ya joto au ya kitropiki.

Ni hatari ya kikazi kwa watu wengi wanaofanya kazi nje au na wanyama, kama vile:

  • Wakulima
  • Wafanyakazi wa migodini
  • Wafanyakazi wa maji taka
  • Wafanyakazi wa machinjio
  • Madaktari wa mifugo na watunza wanyama
  • Wanaojishughulisha na bidhaa za samaki
  • Wafanyakazi wanaotengeneza bidhaa za maziwa
  • Wanajeshi

Ugonjwa huo pia umehusishwa na kuogelea na kuteleza kwenye ziwa na mito iliyochafuliwa.

Kwa hivyo, ni hatari kwa wale wanaoshiriki katika michezo ya nje.

Hatari inaweza kuwa kubwa zaidi kwa wale wanaoshiriki katika shughuli hizi katika hali ya hewa ya joto.

Kwa kuongeza, matukio ya maambukizi ya Leptospirosis kati ya watoto wa mijini yanaonekana kuongezeka.

Tiba ya homa ya Mgunda

Homa ya Mgunda (Leptospirosis) inatibiwa na dawa aina ya antibiotics, kama vile doxycycline au penicillin, ambayo inapaswa kutolewa mapema katika kipindi cha ugonjwa huo.

Zinaweza kuhitajika kwa watu walio na dalili kali zaidi. Watu walio na dalili zinazoashiria leptospirosis wanapaswa kuwasiliana na mtoa huduma wa afya.

Hatari ya kupata ugonjwa huu inaweza kupunguzwa sana kwa kutoogelea au kuzama ndani ya maji ambayo yanaweza kuwa na mkojo wa wanyama, au kutowagusa wanyama walioambukizwa.

Nguo au viatu vya kujikinga vinapaswa kuvaliwa na wale walioathiriwa na maji au udongo uliochafuliwa kwa sababu ya kazi zao au shughuli zao za burudani.