Siku ya hepatitis,WHO yataka mataifa kuweka mikakati kukabili maafa

Umaskini umechangia pakubwa katika kuongezeka kwa idadi ya maafa yanayotokana na ugonjwa huu

Muhtasari

• Wizara ya Afya nchini Kenya imekiri kwamba homa na saratani ya ini ni tatizo kubwa nchini.

• Kufuatia mkurupuko wa janga la Covid-19 raslimali nyingi katika idara ya afya zilielekezwa kufadhili kampeini dhidi ya Covid-19.

Maandamano ya kuadhimisha Siku ya Hepatitis Duniani mwaka huu kutoka bustani ya Uhuru hadi Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta mnamo Julai 28, 2022.
Maandamano ya kuadhimisha Siku ya Hepatitis Duniani mwaka huu kutoka bustani ya Uhuru hadi Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta mnamo Julai 28, 2022.
Image: MAGDALINE SAYA

Shirika hilo limeelezea umuhimu wa kuimarisha huduma za matibabu kwa umma ikiwemo kuleta karibu na wananchi  vituo vya matibabu ili kusaidia katika vita dhidi ya ugonjwa huu hatari. Linalenga kupunguza kiwango cha homa ya ini aina za B na C kwa asilimia 90, kupunguza vifo vinavyohusishwa  na saratani ya ini kwa asilimia 65 na  kuhakikisha kwamba takribani  asilimia 90 ya walioambukizwa wanapata matibabu bora.

Kenya ni miongoni mwa mataifa ambayo raia wake wanakumbwa na hatari ya kuambukizwa homa ya ini. Kulingana na hospitali ya Aga Khan [AKUH], pindi tu mtu anapoambukizwa na virusi hivi, mwili hushindwa kuifadhi  joto na kutoa uchafu mwilini.

Umaskini pia umechangia pakubwa katika kuongezeka kwa idadi ya maafa yanayotokana na ugonjwa huu. Kulingana na Christopher Baraza ambaye alipoteza ndugu kutokana na homa ya ini, ukosefu wa matibabu kutokana na hali ya kutomudu gharama za matibabu kumechangia vifo vingi.

Christopher anasema baada ya nduguye  kuambukizwa, ilikuwa vigumu kwao kumtafutia matibabu kwani familia yake tayari ilikuwa inakabiliwa na changamoto za kukimu mahitaji ya kimsingi.

Kutokana na hali hii, Christopher alimpoteza nduguye  kwa ugonjwa wa saratani ya ini baada ya juhudi za kusaka wahisani kufeli.

Baadhi ya maambukizo ya Hepatitis (homa ya ini) ya virusi yanaweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya ini PICHA/AGENCIES
Baadhi ya maambukizo ya Hepatitis (homa ya ini) ya virusi yanaweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya ini PICHA/AGENCIES

Wizara ya Afya nchini Kenya imekiri kwamba homa na saratani ya ini ni tatizo kubwa nchini hasa kufuatia mkurupuko wa janga la Covid-19 ambapo raslimali nyingi katika idara ya afya zilielekezwa kukabili Covid-19.

Katika maadhimisho ya siku hii shirika la WHO linakumbusha mataifa  kuzidisha juhudi za kukabili ugonjwa wa homa ya ini. 

wananchi wanataadharishwa dhidi ya kupuuza dalili za ugonjwa huu kwa kutembelea vituo vya afya kupimwa na kupokea matibabu.