Rachel Ruto: Mfahamu zaidi mke wa rais mteule wa Kenya

Ruto na Rachel walifunga pingu za maisha na kuanza familia yao changa mwaka 1991.

Muhtasari

•Alizaliwa tarehe 20 mwezi Novemba 1968 mjini Kakamega magharibi mwa Kenya na kupata masomo yake ya sekondari katika shule ya wasichana ya Butere hadi kidato cha sita.

•Wanandoa hao walijaaliwa watoto sita-mabinti watatu na wavulana watatu mkubwa wao akiwa Nick Ruto.

Image: HISANI

Ni mwanamke mtulivu na mnyenyekevu ambaye hutanguliza mapenzi yake kwa Mwenyezi Mungu katika kila hatua yake na kuwakilisha injili

Hulka hii pia inajitokeza katika mtindo wake wa mavazi na hata anavyotoa salamu.

Licha ya umaarufu wa mume wake Wakenya walipata fursa ya kutangamana naye utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ulipoingia madarakani mwaka 2013.

Kutana na Rachel Chebet Ruto, mke wa Rais Mteule wa Kenya William Ruto.

Alizaliwa tarehe 20 mwezi Novemba 1968 mjini Kakamega magharibi mwa Kenya na kupata masomo yake ya sekondari katika shule ya wasichana ya Butere hadi kidato cha sita.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta na kusomea shahada ya Elimu.

Bi Rachel pia alikamilisha shahada yake ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki mwaka 2011.

Japo hakupata nafasi ya kufanya mazoezi ya kufundisha kwa muda mrefu, aliamua kujitosa katika biashara ya utalii ambapo alikuwa akiwapeleka watu kuzuru maeneo tofauti ya ndani na nje ya Kenya.

Familia

Naibu wa Rais Wiliam Ruto na Mke wake Rachel Ruto
Naibu wa Rais Wiliam Ruto na Mke wake Rachel Ruto
Image: HISANI

Bi Rachel na William Ruto walikutana mwanzoni mwa miaka ya tisini na wawili hao walianza kuchumbiana wakiwa chuo kikuu.

Rachel alikuwa akisomea Elimu na mpenzi wake wakati huo alikuwa akisomea Sayansi ya mimea (Botany).

Walifunga pingu za maisha na kuanza familia yao changa mwaka 1991.

Wanandoa hao walijaaliwa watoto sita-mabinti watatu na wavulana watatu mkubwa wao akiwa Nick Ruto.

Rachel Ruto sasa ni mama mkwe wa Mnigeria Dkt Alexander Ezenagu.

Baadhi ya watoto wa Ruto
Baadhi ya watoto wa Ruto
Image: HISANI

Rachel Ruto kama mke wa Naibu wa Rais

Bi Rachel Ruto alikuwa Mke wa naibu wa rais rasmi mwaka 2013, baada ya mume wake Bw William Ruto kuchaguliwa kuwa Naibu wa Rais wa Kenya.

Na tangu wakati huo amekuwa mstari wa mbele kupigania haki ya wanawake na harakati za kuwawezesha katika jamii.

Mpango wake kuwawezesha wanawake kupitia shirika la Joyful Women, uliangaziwa na Televisheni ya Citizen, ambapo alifichua jinsi harakati zake zilivyosaidia idadi kubwa ya wanawake.

Kupitia miradi aliyoanzisha baadhi ya wanawake wameweza kuanzisha biashara, kuweka akiba ya fedha, kununua ardhi na katika mchakato huo kuwajengea imani.

Baadhi ya miradi ya kuwawezesha wanawake ikiwa ni pamoja na:

Uwekezaji kwa wanawake: Huu ni ambao wanawake wengi wanaufahamu kama Table Banking unawawezesha wanawake walioungana 'chamaa' kuweka pesa pamoja kila mwezi au kila wiki na kutokana na fedha hizo kila mwanachama anakopa anachoweza kulipa.

Kabla ya hapo wanawake kwenye chama wamekuwa wakikutana na kuchangisha pesa pamoja na kumpatia mmoja wao kila wiki au mwezi mfumo ambao bado unaeziwa na baadhi yao.

Maji:Huu ulikuwa mpango wa kuwasaidia wanawake kupata maji safi ya matumizi.

Katika shughuli zake za kutangamana na wanawake katika maeneo tofauti nchini mama Rachel aligundua kuwa wanawake wamekuwa wakitembea mwendo mrefu kutafuta maji ndiposa alianzisha mradi huo kwa ushirikiano na serikali.

Kushona: Mradi huu ulianzishwa hususan kuwasaidia wafungwa wanawake: ambao wanawezeshwa kushona, vitambaa ambavyo vinawekwa kwenye fremu na kuuzwa. Pesa zinazotokana na mradi huo wanapewa watakapotoka gerezani.

Pia alianzisha mradi wa ufugaji kuku ambao unasambaza vifaranga kwa wanawake kote nchini kwa bei nafuu.